Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuimarisha zaidi ushirikiano wa kikanda katika kulinda na kusimamizi endelevu wa mazingira na maliasili, ikisisitiza umuhimu wa jitihada za pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuathiri sekta hizo kwa manufaa ya wananchi wote wa Jumuiya.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Mazingira na Usimamizi wa Maliasili (SCENR) wa EAC uliofanyika leo Aprili 23, 2027 jijini Arusha, uliolenga kupitia maendeleo ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 10 wa Kisekta wa Baraza hilo na maamuzi yaliyofikiwa katika mikutano ya nyuma ambayo utekelezaji wake bado haujakamilika.
Akizungumza katika Mkutano huo Mhe. Dkt. Kijaji pamoja na musuala mengine alieleza kuwa licha ya ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali kama misitu, wanyamapori, mito, maziwa makubwa na ukanda wa Bahari ya Hindi, rasilimali hizo zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo; upotevu wa bioanuwai, uchafuzi wa mazingira na matumizi yasiyo endelevu.
“Bila hatua za pamoja na madhubuti, uendelevu wa rasilimali hizi utakuwa hatarini, na hivyo kuhatarisha usalama wa chakula, mapato ya utalii na uimara wa uchumi wa nchi zetu,” alisisitiza Mhe. Dkt. Kijaji
Waziri Kijaji aliendelea kueleza kuwa sekta za uchumi zinazotegemea sekta hizo ikiwemo utalii, kilimo, uvuvi na nishati zinamchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi wanachama na maisha ya wananchi kwa ujumla. Alitoa mfano kuwa, sekta ya utalii pekee katika nchi za EAC inachangia wastani wa zaidi ya asilimia 10 ya pato la taifa (GDP) kwa baadhi ya nchi, huku ikitoa ajira lukuki za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa mamilioni ya Wananchi katika Jumuiya.
Aidha, Mhe. Kijaji amebainisha maeneo mbalimbali muhimu yanayohitaji ushirikiano kuwa ni pamoja na uoanishaji wa sera, sheria na mikakati ya usimamizi wa mazingira, kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha za tabianchi, kuendeleza uchumi wa buluu, mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira na utoaji elimu kwa umma.
Ajenda zingine zilizodaliwa katika mkutano huo ulioanza katika ngazi ya Wataalamu na Makatibu Wakuu kuanzia tarehe 20-22 Aprili 2026, ni pamoja na mabadiliko ya Tabianchi, Maji na Mifumo ya Ikolojia, Uchumi wa Buluu na Bahari, Udhibiti wa Uchafuzi na Makubaliano ya Kimataifa na Ushiriki wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ulijumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Zanzibar, Mhe. Hamis Hassan; Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagirwa; Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew; pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali, ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.







