Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametumia mamlaka yake ya kikatiba kutoa msamaha wa kupunguza adhabu kwa wafungwa 1,369, hatua iliyowezesha wafungwa 436 kuachiwa huru mara moja na wengine 933 kupunguziwa vifungo vyao.

Hatua hiyo imetangazwa leo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobass Katambi ambaye amesema msamaha huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano, kwa kuzingatia Ibara ya 45(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafungwa walionufaika ni pamoja na waliotumikia sehemu ya vifungo vyao kwa mujibu wa sheria, wagonjwa mahututi waliothibitishwa kitaalamu, wazee wenye umri wa miaka 70 na zaidi, pamoja na makundi maalum kama wanawake wajawazito au wenye watoto wachanga gerezani.

Aidha, wafungwa waliokuwa wanatumikia adhabu ndefu, ikiwemo waliokaa gerezani kwa miaka 25 na zaidi au waliokuwa chini ya adhabu ya kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu, pia waliguswa na msamaha huo baada ya tathmini maalum kufanyika.

Hata hivyo, Serikali imeweka bayana kuwa msamaha huo haukuwahusu wafungwa waliopatikana na hatia ya makosa mazito kama vile ugaidi, uharamia, ubakaji, biashara ya binadamu, rushwa, uhujumu uchumi, pamoja na wale wanaotumikia kifungo cha maisha au waliowahi kunufaika na msamaha wa Rais hapo awali.

Katika hatua nyingine, Serikali imesisitiza kuwa lengo la msamaha huo ni kutoa fursa ya pili kwa wafungwa waliorekebika kurejea katika jamii na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.

“Ni matarajio ya Serikali kuwa wale walioachiwa huru watarejea katika jamii wakiwa na nidhamu, wakijihusisha na shughuli halali za kiuchumi na kuepuka kurejea kwenye vitendo vya uhalifu,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hatua hiyo imepokelewa kama ishara ya huruma na dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha haki, utu na marekebisho ya wafungwa nchini, sambamba na kupunguza msongamano magerezani na kuimarisha mfumo wa marekebisho ya tabia.

Maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yameendelea kuakisiwa na hatua mbalimbali za kijamii na kiuchumi zinazolenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa na ustawi wa wananchi.