Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, Mwalimu Mwajuma Nyamka, ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za Mitaa na chama ngazi ya chini kuwafikia wananchi, kuwahudumia pamoja na kuwapa taarifa kuhusu mipango ya serikali na mafanikio ya utekelezaji wa Ilani.
Nyamka ametoa wito huo April 28,2026 katika kata ya Mailmoja wakati akihitimisha ziara yake ya kata kwa kata katika kata 14, akisisitiza umuhimu wa kuacha mijadala ya uchaguzi na kuelekeza nguvu katika shughuli za maendeleo.
“Uchaguzi umekwisha, ukiona hadi leo kuna mtu bado anazungumzia uchaguzi au kuunda makundi, bado atakuwa na shida, kwa sasa tufanye kazi za maendeleo, tufike kwa wananchi, tusikilize na tutatue changamoto zao,” alisema Nyamka.
Nyamka alisema ziara hiyo ililenga kuwashukuru wananchi kwa kuendelea kukiunga mkono chama na kukipatia ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akielezea umuhimu wa uwajibikaji na ushirikiano ili kuharakisha maendeleo.
Katika hatua nyingine amehamasisha uandikishaji wa wanachama wapya na ulipaji wa ada ili kukiimarisha chama.
Pia amempongeza Rais dkt Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake imara katika kusimamia utekelezaji wa Ilani na kudumisha amani nchini, akisema Tanzania inaendelea kubaki kisiwa cha amani.
Wakati huo huo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Kibaha Mjini, Zuhura Sekelela, amesihi wanawake kujiunga kwenye vikundi ili kunufaika na mikopo ya halmashauri, huku akitoa wito kwa wanufaika wa mikopo hiyo kuirejesha kwa wakati ili kuwawezesha wengine kunufaika.
Akizungumzia changamoto za kata hiyo, Katibu Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Hassan Suleiman, alielezea kuwa ubovu wa barabara za ndani na barabara ya Sheli–Muheza hadi Msufini ni miongoni mwa kero kubwa katika kata ya Mailmoja, huku akieleza kuwa kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi.
Aliongeza kuwa katika mpango huo kutajengwa kituo cha afya katika mtaa wa Muheza, ujenzi wa jengo la utawala na bwalo katika Shule ya Sekondari Bundikani, vyumba saba vya madarasa katika Shule ya Msingi Muheza na vyumba 15 pamoja na matundu 20 ya vyoo katika Shule ya Msingi Maendeleo.







