Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umechukua hatua madhubuti ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kuwagawia watumishi wake majiko ya umeme, ikiwa ni sehemu ya juhudi za makusudi za kuhamasisha mabadiliko ya matumizi ya nishati nchini.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa PBPA, Mhandisi Bruno Tarimo, amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha juhudi za taasisi katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi na salama kwa matumizi ya kila siku.

Ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia sera mbalimbali za kitaifa na kimataifa, imeendelea kutambua umuhimu wa nishati safi ya kupikia kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na changamoto za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi.

“PBPA inatekeleza jukumu muhimu katika kusaidia juhudi za Serikali za kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Ugawaji wa majiko janja aina ya pressure cooker kwa watumishi ni sehemu ya mkakati huo,” amesema Tarimo.

Aidha, amewataka wanufaika wa majiko hayo kuyatumia ipasavyo na kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika jamii zao ili kuongeza uelewa na kuharakisha mabadiliko ya matumizi ya nishati nchini.

Kwa upande wake, Afisa Dawati wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka PBPA, Bi. Hilda Kowero, amesema kuwa Serikali imeweka mkakati maalum wa nishati safi ya kupikia unaolenga kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.

Amefafanua kuwa matumizi ya majiko ya umeme husaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hivyo kulinda misitu, kupunguza ukataji wa miti na kuboresha afya kwa kupunguza madhara ya moshi yanayosababisha magonjwa ya njia ya hewa.

Katika kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya majiko hayo, watumishi walipatiwa mafunzo maalum kuhusu namna bora ya kuyatumia, kutunza na kuzingatia tahadhari za usalama. Mafunzo hayo yalijumuisha matumizi sahihi ya umeme, njia za kupunguza matumizi ya nishati, pamoja na mbinu za kupika kwa ufanisi kwa kutumia majiko ya shinikizo (pressure cooker). Hatua hiyo inalenga kuwajengea watumishi uelewa wa kina ili waweze kunufaika kikamilifu na teknolojia hiyo na kueneza maarifa hayo kwa jamii inayowazunguka.

Bi. Kowero ameongeza kuwa PBPA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha mabadiliko ya tabia kwa wananchi ili kuongeza matumizi ya nishati safi na kuchangia katika ujenzi wa jamii yenye afya bora na mazingira endelevu.