Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa Mkoa wa Dodoma una fursa nyingi za kiuchumi na kijamii katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, biashara, utalii na madini ambazo zikiendelezwa na kuchangamkiwa ipasavyo zitakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi na watu wake.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ofisini kwake jijini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha, baada ya hivi karibuni kuteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa Waziri wa Fedha.
Alisema kuwa Mkoa wa Dodoma uko katikati ya nchi na unaweza kutumika ipasavyo kama kitovu ama kituo cha biashara kwa kuunganika na mikoa mingine kimkakati ikiwemo bandari kavu kwa ajili ya kuhifadhi na kusafirisha makontena na bidhaa nyingine Kwenda maeneo mengine ya ndani na nje ya nchi.
“Lakini pia tuna fursa kubwa ya kilimo ambayo imeajiri watanzania wengi zaidi, mazao tofauti, fursa ya utalii lakini kubwa zaidi ni fursa ya madini ambapo mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa miongoni mwa mikoa yenye utajiri wa madini ambayo yakichanganywa na madini kutoka mikoa mingine yakaongezewa thamani, wananchi wanaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa na fursa hizo” alisema Mhe. Balozi Omar.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, alimweleza Mhe. Balozi Omar kuwa mkoa huo sasa umepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwamba mikakati mbalimbali inaelekezwa katika kukuza zaidi biashara, utalii, sekta ya madini, kilimo, pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma za jamii.
Alitoa wito kwa wadau mbalimbali kutoka Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kuwekeza mkoani humo ikiwemo ujenzi wa vituo vya Kimataifa vya mikutano, hoteli za hadhi ya nyota tano, pamoja na kuchakata madini ambayo alisema yako lukuki mkoani mwake.
Katika Kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma aliambatana na Katibu Tawala wa mkoa huo, Dkt. Khatibu Kazungu.



