Na Theophilida Felician, JamhuriMedia, Kagera.
Mchungaji wa Kanisa la T.A .G lililopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Bruno Athazi amekea vikali changamoto ya migogoro ya ndoa ambayo imekuwa chanzo cha matukio mbalimbali ya kikatili katika jamii.
Mchungaji Bruno ametoa kauli hiyo akiendesha ibada ya mazishi ya mwenyekiti wa Shirika la Wanaume Wanaopitia changamoto katika ndoa kwa upande wa Mkoa Kagera SHIWACHANDO, Richard Leornad Mshashu tukio lililofanyika mtaa wa Busisi kata Kibeta Manispaa ya Bukoba.
Amesema kuwa kumekuwepo na matukio kadhaa ndani ya wanandoa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa uelewano unaotengeneza migogoro ya muda mrefu inayochochea matukio ya namna hiyo.
Amevitaja baadhi ya vitu vinavyopelekea mifarakano ni pamoja na ulevi, usaliti, fitina mali, na ugomvi usioisha hadi kusababisha baadhi ya wana ndoa kutishiana kwa kauli ya kuuana hadi wengine kuishi kwa kutengana wakiwa ndani ya nyumba moja jambo ambalo amelitaja kuwa hatarishi.
Kutokana na changamoto hiyo amesema kwamba kumekuwa na matukio hasa hasa kunyanyasika pande zote mbili mke au mme kuuana, kuuliwa na mengine mengi amesisitiza kuwa misingi ya ndoa ni amani na upendo hivyo inapaswa kuheshimiwa na watu wote.
Aidha ameiasa jamii kumurudia mwenyezi Mungu kwa kutenda matendo yaliyo mema nyakati zote na kuepukana na matendo maovu kwani kila binadamu anapaswa kuitengeneza njia akiwa bado hai hapa Duniani.
Kifo cha mwenyekiti Rechard Leonard Mshashu kilichotokea Tarehe 11 Mai 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Bukoba kimeacha simanzi kubwa kwa wanashirika la SHIWACHANDO, ndugu, wadau na wananchi kwa ujumla.




