Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dar es Salaam
SERIKALI imesema inapambana na haitamuonea haya mtu yoyote muharibifu wa mazingira na kuitaka jamii kulinda na kutunza mazingira kwa kuwa yana umuhimu mkubwa kiuchumi na kimaendeleo.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Reuben Kwagilwa, wakati wa mafunzo kwa waandishi wa Habari kuhusina na faida za biashara ya kaboni yaliyoandaliwa na Kituo cha Taifa ya Uratibu Kaboni Tanzania (NCMC).
Kwagilwa alisema kuwa Serikali inaendelea kusimamia suala la utunzaji mazingira kikamilifu na itahakikisha inafanya uwekezaji na miradi bila ya kuzingitia hilo.
“Serikali inaendelea kusimamia suala la utunzaji mazingira hivyo haitomuonea aibu mtu yeyote ambaye atabainika kuharibu mazingira kwani ni sawa na kurudisha nyuma shughuli za maendeleo.
“Kuna umuhimu mkubwa wa kulinda mazingira kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tibia ya nchi pia kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi kushiriki kikamilifu ili kupunguza uharibifu wa mazingira ambao husababisha ukame na kupoteza rasilimali nyingi” alisema Waziri Kwagilwa.
Kwagilwa alisema kuwa shughuli nyingi zinazofanywa na binadamu za kiuchumi na maendeleo zimesababisha athari za mazingira na zimechangia mabadiliko ya tabia ya nchi.
Waziri Kwagilwa alimpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwa kiongozi mkuu wa utunzaji mazingira. “Hii ya utunzaji wa mazingira Rais Dk.Samia amejijengea umaarufu mkubwa katika utunzaji wa mazingira duniani,”alisema.
Alisema sehemu kubwa duniani kwa nyakati tofauti imefanya mikutano na kusaini makubaliano mbalimbali ya tabia ya nchi.

Aidha alisema kuna njia mbili za kukabiliana na mabadiliko hayo ambayo ni uhimilivu wa mazingira ili mazingira yaweze kuhimiri na nchi itakuwa imeweza kupunguza kiwango cha gesi joto kinachokwenda kwenye ikolojia ya dunia.
Alizitaja njia hizo kuwa ni upandaji wa misitu,kulinda vyanzo vya maji na kufanya kilimo endelevu kinachozingatia utunzaji wa mazingira.
Akizungumzia biashara kaboni Naibu Waziri alisema wananchi wasitunze misitu kwa mazoea bali wapande miti kwa ajili ya kuingiza kipato kutokana na biashara ya kaboni.
Alisema serikali inaamini kuwa kama waandishi wa habari wakielewa vizuri nayo jamii, kampuni au taasisi kupitia kalamu zao namna ambavyo biashara ya hewa ya kaboni unavyofanyika na faida zake, taasisi zinavyoweza kuendesha biashara ya kaboni.
Naye Mkurugenzi wa NCMC, Kathryn Kigaraba alisema kituo hicho kitaendelea kuratibu biashara ya kabon na kuhakikisha Tanzania inachangia kwenye masoko ya kimataifa ya biashara hiyo.
Pia alisema kituo kinatarajia waandishi wa habari watakuwa mstari mbele kuongeza uelewa kwa jamii kuhusiana na fursa mbalimbal zinazopatikana katika biashara ya kaboni.
“Natumai mtasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa miradi ya kaboni na kusambaza taarifa sahihi na kwa wakati,”alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masuala ya Upimaji ,Uhakiki, Usajili na Tathimini ya Gesi Joto, Deo Shirima, kutoka CMNC, alisema biashara ya kaboni inalenga kutoa motisha kwa ajili ya shughuli zote zinazolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na thari zake kwa lengo la kuweka ustahimilivu au usimamizi endelevu wa mazingira katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii ambapo inaweza kufanywa na kampuni, taasisi na mtu binafsi.
“Biashara hiyo inaweza kufanywa katika sekta ya taka ,kilimo mseto,matumizi ya viwanda,usafiri endelevu,uhifadhi misitu,matumizi ya nishati safi kwa kupunguza ongezeko la gesi joto au kuondoa kiwango cha nyuzi joto” alisema.
Alisema hadi sasa kuna jumla ya miradi 99 iliyosajiliwa katika kituo hicho na tayari kampuni nane zimeanza utekelezaji .






