Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam.
Kampuni ya Itrust Finance limited imezindua rasmi hatifungani yake ikiwa ni hatifungani ya kwanza nchini kutolewa na kampuni wakala wa soko la hisa na msimamizi wa mifuko ya uwekezaji nchini tanzania.
Hatifungani hiyo ni ya muda wa kati (medium-term note (mtn) programme) yenye thamani ya shilingi bilioni 100.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika 19 may 2026 katika hotel ya HYATT (Kilimanjaro Hotel )Ofisa mtendaji mkuu wa Itrust Finance limited Faiz Arab amesema kuwa awamu ya kwanza ya program inalenga kukusanya shilingi bilioni 15 ikiwa na nyongeza ya shilingi bilioni 5 kupitia chaguo la ziada.
Ambapo wawekezaji wanatarajiwa kupata riba shindani ya asilimia 13 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mine,
Amesema kuwa riba ya hatifungani hiyo italipwa kila baada ya miezi mitatu bila kukatwa kodi (withholding tax) jambo linalolenga kuwapa wawekezaji mapato ya uhakika na yanayotabirika, anasema.
‘’Muundo wa hatifungani umeandaliwa kwa namna inayowavutia wawekezaji wa aina mbalimbali huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwekwa kuwa shilingi 500,000 ili kutoa nafasi kwa wawekezaji binafsi na taasisi kushiriki kwa urahisi.

Aidha hatifungani itakuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo riba shindani yenye kiwango kisichobadilika msamaha wa kodi ya zuio kwenye riba pamoja na kuongeza fursa ya uwekezaji kupitia dhamana za mapato yasiyobadilika (fixed income investments)’’Amesema
Amesema muda mfupi wa ukomavu wa miaka minne pamoja na mfumo wa malipo ya kila robo mwaka vinaifanya Itrust Bond kuwa mbadala wenye mvuto ukilinganishwa na dhamana za kawaida za serikali.
Pia fedha zitakazopatikana kupitia utoaji wa hatifungani hiyo zitatumika katika kutekeleza mipango mbalimbali ya kimkakati ikiwemo kuongeza uwezo wa utoaji mikopo, kuwekeza katika majukwaa ya kidijitali ya kisasa pamoja na kuimarisha mtaji wa uendeshaji wa kampuni kwa ajili ya kukuza shughuli zake,
Amesema katika kurahisisha usajili wa itrust bond namna rahisi ya kuwekeza kupitia uzinduzi wa programu ya simu ya itrust app,programu hiyo ya kipekee itawawezesha watumiaji kuwekeza katika hatifungani, hisa na mifuko ya uwekezaji huku wakifuatilia uwekezaji wao wote katika sehemu moja.
‘’ITrust Finance limited ni Taasisi ya huduma za kifedha ya daraja la pili (tier 2) iliyoidhinishwa na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na CMSA.

Kampuni hiyo hutoa huduma mbalimbali za kifedha zikiwemo uwakala wa soko la hisa, ushauri wa uwekezaji, usimamizi wa mifuko ya uwekezaji pamoja na huduma za mikopo ya kawaida na inayozingatia misingi ya shariah kupitia kitengo chake cha imaan finance.
Kwa kuzingatia nafasi yake kubwa sokoni na kuendelea kujijengea sifa kama mshirika wa kuaminika katika uwekezaji, itrust inalenga kutumia programu hii kuongeza ushiriki wa wananchi katika masoko ya fedha nchini huku ikiunga mkono ukuaji wa uchumi shirikishi.
Wawekezaji wanaweza kupata taarifa zaidi na kuwasilisha maombi ya kuwekeza katika hatifungani hiyo kupitia majukwaa ya kidijitali ya Itrust ikiwemo aplikesheni, tovuti na mfumo wa mtandaoni wa kampuni
hiyo’’Amesema.
Afisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana (cmsa) CPA. Nicodemus Mkama amesema Utoaji wa hatifungani ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha yaani Financial Sector Development Master Plan 2020/21 na 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.
“Hatifungani hii inawezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo yaani Tanzania Development Vision 2050 (DIRA 2050) yenye lengo la kuwa na uchumi shindani, himilivu na jumuishi kwa maendeleo endelevu kwa Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na kukuza sekta ya ujasiriamali.

Masoko ya Mitaji nchini ni imara, himilivu na yanaendelea kushamiri huku mamlaka ya Masoko ya Mitaji na dhamana (CMSA) itaendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuchagiza na kujenga uchumi
shindani kwa maendeleo ya watu’’alisema.
Alidai makampuni na taasisi katika sekta binafsi na umma zinatakiwa kutumia fursa katika masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza shughuli za kukuza na kuendeleza biashara na miradi ya maendeleo.
Ambapo kampuni zenye leseni ya kutoa huduma katika masoko ya mitaji kuendeleza mikakati ya kuanzisha bidhaa bunifu zinazopanua na kuongeza fursa kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.


