Hali ya ulinzi na usalama katika mipaka ya Tanzania imeendelea kuwa shwari katika mwaka wa fedha 2025/26 licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiusalama na miundombinu katika baadhi ya maeneo ya mipakani.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Bungeni jijini Dodoma jana, Waziri wa Ulinzi Dkt. Rhimo Nyansaho alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimeendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha usalama wa mipaka yote ya nchi unaimarishwa.
Alisema Tanzania ina mipaka yenye urefu wa kilomita 5,923.41 inayohusisha mipaka ya nchi kavu, anga na eneo la maji, huku ikipakana na nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Uganda, Zambia pamoja na mipaka ya Bahari ya Hindi inayohusisha Comoros na Shelisheli.

Dkt.Nyansaho alisema katika kipindi husika hakukuwa na matukio yaliyoashiria uvunjifu wa amani kati ya Tanzania na nchi jirani, ingawa baadhi ya mipaka imeendelea kukabiliwa na changamoto za uharibifu wa alama za mipaka, ukosefu wa barabara za ulinzi na migogoro ya ndani katika baadhi ya nchi jirani.

Alieleza kuwa mpaka wa Tanzania na Burundi wenye urefu wa kilomita 468.85 umeendelea kuwa salama, licha ya changamoto za uharibifu wa alama za mpaka na barabara za ulinzi zinazoathiri shughuli za kiusalama.

Kwa upande wa mpaka wa Tanzania na DRC wenye urefu wa kilomita 554, Waziri huyo alisema hali ya usalama ni shwari, lakini mapigano yanayoendelea mashariki mwa DRC kati ya jeshi la nchi hiyo na makundi yenye silaha, hususan kundi la M23, yanaendelea kuwa changamoto ya kiusalama katika eneo hilo.

Alisema kundi hilo limeendelea kushikilia maeneo ya kimkakati katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, hali inayoongeza tahadhari ya kiusalama katika mpaka huo, huku JWTZ ikiendelea kufanya doria za mara kwa mara kufuatilia hali hiyo.

Aidha, alisema mpaka wa Tanzania na Kenya wenye urefu wa kilomita 1,187 umeendelea kuwa salama na kazi ya kuimarisha alama za mpaka inaendelea kupitia ushirikiano wa wataalamu kutoka Tanzania na Kenya.

Katika mpaka wa Tanzania na Malawi wenye urefu wa kilomita 394, Dkt.Nyansaho alisema hakuna tukio lililoripotiwa kuhatarisha usalama wa nchi, ingawa changamoto ya mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa bado inaendelea kushughulikiwa kwa njia za kidiplomasia kupitia Tume Maalum ya Usuluhishi chini ya Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano.

Kwa upande wa mpaka wa Tanzania na Msumbiji wenye urefu wa kilomita 922.76, Waziri huyo alisema changamoto kubwa ni uwepo wa kikundi cha kigaidi cha Ansar Al-Sunna Wal Jamaah (ASWJ) kinachohusishwa na Islamic State Mozambique Province katika Jimbo la Cabo Delgado.

Alisema Serikali imeendelea kuimarisha ulinzi katika eneo hilo kwa kuvijengea uwezo vikundi vya JWTZ kupitia vifaa na zana mbalimbali za kisasa ili kuhakikisha usalama wa wananchi unaendelea kudumishwa.

Dkt.Nyansaho pia alisema mipaka ya Tanzania na Rwanda, Uganda pamoja na Zambia imeendelea kuwa salama licha ya changamoto za uharibifu wa alama za mipaka na migogoro midogo ya kiutawala inayoshughulikiwa kupitia njia za kidiplomasia.

Kuhusu ulinzi wa anga la juu, alisema hali imeendelea kuwa shwari licha ya kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia ya kisasa ambayo imeifanya sekta hiyo kuwa na changamoto mpya za kiusalama.

Aidha, alisema katika Bahari ya Hindi yenye urefu wa Nautical Miles 864.376, JWTZ imeendelea kufanya doria za mara kwa mara kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kuzuia uharamia, wahamiaji haramu, uvuvi haramu, biashara ya dawa za kulevya pamoja na vitisho vya kigaidi.

Katika hatua nyingine, Waziri Nyansaho alisema Serikali katika mwaka wa fedha 2026/27 inatarajia kutenga jumla ya Shilingi 4,286,489,324,427.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Maendeleo ya Wizara ya Ulinzi.

Alisema fedha hizo zitaelekezwa katika kuimarisha uwezo wa JWTZ, kuboresha miundombinu ya ulinzi, vifaa vya kisasa pamoja na mafunzo ya kitaalamu kwa maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Akizungumzia mafunzo ya Usalama na Stratejia, Dkt.Nyansaho alisema Wizara kupitia Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC) imeendelea kutoa mafunzo kwa maafisa waandamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na watumishi wa umma katika ngazi za kisera na kistratejia.

Alisema mafunzo hayo yanahusisha ushirikiano wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini, Bangladesh, Botswana, Burundi, China, Ethiopia, India, Kenya, Malawi, Misri, Namibia, Nigeria, Rwanda, Sierra Leone, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Aidha, alisema ushiriki wa nchi hizo unaonesha ubora wa kimataifa wa mtaala wa Chuo hicho pamoja na mchango wa Tanzania katika kuimarisha diplomasia ya ulinzi na ushirikiano wa kimataifa.

Dkt.Nyansaho alisema katika mwaka wa fedha 2025/26 Chuo hicho kiliendesha mafunzo kwa viongozi waandamizi wa Serikali na sekta binafsi kuanzia Machi 9 hadi 13, 2026, yakijikita katika mada ya “Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika Kuchochea Maendeleo Endelevu ya Taifa.”

Aliongeza kuwa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC) pamoja na Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) vimeendelea kuendesha mafunzo kwa kushirikiana na nchi mbalimbali ili kuimarisha uhusiano wa kijeshi na diplomasia ya ulinzi.