Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeongeza mtandao wa barabara za lami nchini hadi kufikia kilometa 12,225.26, hatua inayotajwa kuendelea kuimarisha uchumi na huduma za usafiri katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma Mei 20, 2026, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema ndani ya kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026 Serikali imejenga kilometa 243.13 za barabara za lami pamoja na kufanya ukarabati wa kilometa 94.36 kwa kiwango cha changarawe.
Amesema mtandao wa barabara za kitaifa unaosimamiwa na TANROADS kwa sasa una jumla ya kilometa 37,734.41 huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika ujenzi na matengenezo ya miundombinu hiyo muhimu.
Kwa mujibu wa Ulega, wakati Tanzania inapata uhuru mwaka 1961 kulikuwa na kilometa 1,360 pekee za barabara za lami, lakini kuanzia Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi ya Tano zilijengwa kilometa 9,369.81.
Aidha amesema katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, zimejengwa kilometa 1,495.45 za barabara pamoja na madaraja makubwa 18.
“Maendeleo haya yanaendelea kufungua fursa za kiuchumi na kuongeza ufanisi wa sekta nyingine za usafiri ikiwemo reli, bandari na viwanja vya ndege,” amesema Ulega.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja makubwa tisa huku madaraja 11 yakiendelea kujengwa na maandalizi ya ujenzi wa madaraja mengine 13 yakiendelea.
Pia amesema Serikali imeendelea kulinda uwekezaji wa miundombinu hiyo kwa kufanya matengenezo mbalimbali ambapo katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, matengenezo ya kawaida yamefanyika katika kilometa 16,782.58 za barabara, matengenezo ya muda maalum kwa kilometa 1,101.12 pamoja na maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 147.13 na madaraja 1,383.
Amesema hatua hizo zina lengo la kuhakikisha barabara na madaraja vinabaki salama, vinadumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.




