Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imeomba kuidhinishiwa Sh trilioni 2.5 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele sita vikuu vinavyolenga kuimarisha miundombinu ya usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alisema Serikali itaendelea kuelekeza nguvu katika ujenzi wa barabara, madaraja na miundombinu mingine ya kimkakati ili kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.

Amesema uwekezaji huo utawezesha kupunguza changamoto za usafiri katika maeneo yanayokatika wakati wa mvua, kupunguza gharama za usafirishaji pamoja na kuongeza ufanisi wa usafiri wa bidhaa na huduma ndani na nje ya nchi.

Pia ameeleza Serikali itaendelea kujenga miundombinu inayoweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa katika ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko.

“Miundombinu bora ni msingi wa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi, hivyo Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi yenye tija kwa Taifa,” amesema.

Katika mpango huo, Serikali imepanga kuendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara kuu na za mikoa kwa kiwango cha lami na changarawe, sambamba na ujenzi wa madaraja makubwa, madogo na makalavati ili kuimarisha mawasiliano kati ya maeneo mbalimbali nchini.

Waziri huyo alisema matengenezo ya barabara na madaraja yaliyopo yataendelea kufanyika ili kuhakikisha miundombinu hiyo inabaki salama na kudumu kwa muda mrefu.

Aidha, Serikali imeweka mkazo katika kukamilisha miundombinu iliyoharibiwa na mvua za El-Nino pamoja na Kimbunga Hidaya ili kurejesha huduma za usafiri katika maeneo yaliyoathirika.
Katika hatua nyingine, wizara hiyo itaendelea na upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa miradi mipya ya barabara na madaraja ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya baadaye.

Serikali pia imeeleza dhamira ya kupunguza msongamano wa magari katika majiji ya Dar es Salaam na Dodoma kupitia upanuzi wa barabara, ujenzi wa flyover na barabara za mzunguko.

Kwa upande wa Dar es Salaam, amesema miradi ya kupunguza msongamano wa magari inaendelea ikiwemo upanuzi wa baadhi ya barabara na maandalizi ya ujenzi wa flyover katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Aidha, Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa expressway ya Kibaha–Chalinze–Morogoro pamoja na barabara zinazounganisha vituo vya reli ya kisasa ya SGR.

Katika sekta ya ajira, Waziri huyo amesema miradi ya ujenzi imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania ambapo jumla ya nafasi 18,988 zilitolewa mwaka 2025 kwa vijana, wanawake na mafundi wa kada mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso amesema kuna umuhimu wa Serikali kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inasimamiwa kwa karibu ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Amesema kamati hiyo pia imeishauri Serikali kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya ujenzi pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.