*Yajipanga kutekeleza maazimio ya Jukwaa la Miji Afrika na Kushiriki Mapitio ya Ajenda Mpya ya Miji Julai 2026
Na Mwandishi Wetu
Tanzania imeunga mkono Azimio la Nairobi kuhusu Makazi na Maendeleo Endelevu (Nairobi Declaration for Sustainable Housing and Development) pamoja na kuahidi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa maazimio hayo yanayolenga kuimarisha maendeleo endelevu ya miji barani humo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia mkutano uliojadili utekelezaji wa Azimio la Nairobi na Ajenda mpya ya Miji Afrika ambapo washiriki walijadili namna ya kugeuza azimio hilo kutoka ahadi za kisiasa kuwa utekelezaji wa vitendo kupitia mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini.
Katika mkutano huo uliofanyika 19 Mei, 2026 pembezoni mwa Kongamano la 13 la Jukwaa la Miji Duniani (13th World Urban Forum), Tanzania pia ilieleza utayari wake wa kushiriki mkutano wa ngazi za juu wa mapitio ya Ajenda Mpya ya Miji unaotarajiwa kufanyika mwezi Julai 2026 jijini New York, Marekani, chini ya Umoja wa Mataifa.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na utekelezaji wa Azimio la Nairobi baada ya Jukwaa la Pili la Miji Afrika, umuhimu wa Afrika kuwa na sauti moja katika mapitio ya Ajenda Mpya ya Miji ya Umoja wa Mataifa pamoja na kuingiza masuala ya makazi na maendeleo ya miji katika mipango ya maendeleo ya kitaifa na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, kikao hicho kilikubaliana kutumia mfumo wa tathmini wa Umoja wa Afrika (African Union Implementation Scorecard) kufuatilia utekelezaji wa maamuzi katika maeneo sita ya kisiasa huku Azimio la Nairobi likipitishwa kuwa mfumo mkuu wa bara la Afrika katika maendeleo endelevu ya miji.
Katika mkutano huo, Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe.
Katika hatua nyingine, Tume ya Umoja wa Afrika imepewa jukumu la kuratibu utekelezaji wa mfumo huo wa ufuatiliaji kwa kushirikiana na sekretarieti ya Kamati Maalum ya Kitaalam inayosimamia Utawala Bora, Serikali za Mitaa na Maendeleo ya Miji (STC -8) huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi duniani, UN-Habitat, likitarajiwa kuanzisha Programu ya Makazi Nafuu Afrika pamoja na mfumo wake wa utekelezaji.
Nchi wanachama pia zimeelekezwa kuoanisha mipango yao ya maendeleo na malengo ya Maendeleo Endelevu hususani lengo la 11 (SDG 11 ) na Agenda 2063, kuwasilisha taarifa za maendeleo ya miji kila mwaka na kufanya mapitio ya sera za makazi na maendeleo ya miji kulingana na mazingira ya bara la Afrika.



