*Asema wasingemtakia mema, maisha yote amekulia kwao *Ndiye mwasisi jina Kagera
Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Pius Ngeze, amefichua siri namna alivyogoma kuhamishiwa Wilaya ya Chato mkoani Geita wakati wa mchakato wa kuundwa mkoa mpya mwaka 2012.
Kabla ya kuanzishwa Mkoa mpya wa Geita, eneo hilo lilikuwa sehemu ya mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera, jambo ambalo amesema lilimpa wakati mgumu kwa sababu amezaliwa, kukulia na kusomea mkoani Kagera.
“Kuna wakati kulikuwa na vuguguvu la kutaka kunipeleka Chato, nikasema ooooh! Hawa watu hawanitakii mema, maisha yangu yote yamekuwa Kagera, sasa wananipeleka Chato, si wanataka kunimalizia heshima? Maisha yangu yote nimekuwa hapa, nimesomea elimu ya msingi, nimefanya utafiti wangu wa chuo kikuu hapa hapa, hata nilipokamilisha bado Kagera ilikuwa imo ndani.
“Nilianza uongozi Kagera, sasa unaniambia niende mkoa mpya, kwa kweli ilikuwa inaniumiza kidogo. Ninamshukuru Mungu alitusaidia sikwenda Chato na sitakwenda, hili limekwisha. Tulipambana mno, haikuwa rahisi kujenga hoja,” amesema Ngeze.
Akizungumza wakati wa mahojiano na mtandao wa The Voice mjini Bukoba mwishoni mwa wiki, Ngeze amesema
alichelewa kuanza masomo yake mapema kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi ya kifamilia enzi hizo.
“Mama yangu alizaa watoto saba, lakini wa kike walikuwa wanafariki dunia kutokana na malaria, nilifanya kazi zote za kupika, kukata majani, kufyeka na mengine mengi.
“Hali hii ilisababisha nichelewe kuanza masomo, hapa Munganza kulikuwa na shule mbili zilizofunguliwa mwaka 1953, Munganza na Buyimbogo ambayo ilikuwa ya misheni.
“Nakumbuka wakati ule baba alikuwa akienda sana nchi jirani ya Uganda, alikuwa akimuacha mama. Mimi nilikuwa mtoto wa kwanza, hivyo siku zote mama alikuwa anahangaika kunipeleka shuleni asubuhi. Ulifika wakati akanipangishia kwa jamaa mmoja kule Buyimbogo. Alichoka kuwa ananipeleka,” amesema.
Amesema kutokana na kuchoka, mama yake alimuomba kiongozi wa serikali hapo hapo Munganza ili mwanae arudi kusomea nyumbani, hiyo ilikuwa mwaka 1954, lakini alikataliwa.
“Mwaka huo huo alikataliwa na kuambiwa kwamba ‘hatupokei mwanafunzi mwaka huu hadi mwaka kesho’, mimi nikaenda kuanza upya darasa la kwanza nikiwa na umri wa miaka 11. Wakati ule hakukuwa na shule nyingi, tulisubiri zijengwe, kwa bahati nzuri tungechelewa kidogo nisingesoma kabisa.
“Basi nikasoma pale Munganza miaka mitatu, nikachaguliwa kwenda Middle School, nilisoma darasa la tano, sita, saba mpaka la nane, nilihitimu mwaka 1961, wakati nchi yetu inapata uhuru. Niliingia kidato cha kwanza mwaka 1962, wakati ule kupata nafasi ya kwenda kidato cha kwanza ilikuwa ni bahati kweli kweli. Kwa Wilaya ya Ngara tulichaguliwa watoto tisa tu, nakumbuka nilipangiwa Ihungo Sekondari.
“Pale niliungana na wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali, wengi wao wa Bukoba, nikasoma, nilikuwa na uwezo mkubwa wa akili, mwisho wa mwaka walimu walipofanya tathmini walinivusha kutoka kidato cha kwanza hadi cha tatu. Nilipoingia hapo niliongoza vizuri, hakika ninamshukuru Mungu sana, nilihitimu Ihungo mwaka 1966,” amesema.
Amesema baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda ambako alihitimu mwaka 1970.
“Baada ya kuhitimu niliajiriwa kama ofisa mipango, Wizara ya Kilimo, hapa nilifanya kazi kama miaka miwili hivi, mwaka 1972, serikali ilianzisha mfumo mpya wa uongozi ulioitwa ‘kupeleka madaraka mikoani’, nikawa miongoni mwa maofisa wa kwanza kuteuliwa na Rais Julius Nyerere kuwa ofisa mipango Wilaya ya Iringa mwaka 1976.
“Nilichapa kazi sana pale Iringa, Nyerere akanipenda. Mwaka 1975, niliteuliwa kuwa Kamishna wa Mipango na Udhibiti Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, nikahama Iringa nikaenda Dodoma, nikachapa kazi kwelikweli kwenye cheo hiki kipya kwa miaka miwili,” amesema.

Amesema mwaka 1977, alishawishiwa na ndugu na marafiki zake kuingia kwenye ulingo wa siasa ambaako alikwenda kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa na kushinda nafasi hiyo akiwa na umri wa miaka 34.
“Hapo nilianza kuongoza chama na serikali, niliongoza mpaka mwaka 1992 ulipoingia mfumo wa vyama vingi. Nilijitahdi mno, nilikuwa ninachaguliwa kila baada ya miaka mitano ninashinda. Mwaka 1995 nilikwenda kugombea ubunge Jimbo la Ngara nikachaguliwa. Nikiwa mbunge mwaka 1997 muda wangu wa kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa ulimalizika, sikugombea tena.
“Niliendelea kuwatumikia wananchi wa Ngara hadi mwaka 2000. Niligombea tena lakini kura hazikutosha, nikastaafu siasa.
“Aliingia mwenyekiti mwingine ambaye baadaye alipata matatizo, nikaombwa nigombee tena nikakataa, nikasema ukirudi utashindwa. Kulikuwa na mzee mmoja Kachambwa (marehemu sasa), alikuwa anaitwa profesa, alinishawishi mno na kuniambia sishindwi…basi nikaingia kazini tena, nikaanza kampeni, nikashinda uenyekiti awamu ya pili, kitu ambacho si cha kawaida.
“Waliniita na kunipa kazi moja kubwa mno ya kwenda kukomboa majimbo mawili ambayo yalikuwa yamechukuliwa na wapinzani – Jimbo la Bukoba Mjini na Kyerwa, huu ndio ulikuwa mkakati wa kwanza. Hiki ndicho kilikuwa kigezo kikubwa kuwa chama kilikuwa kinanihitaji nikarudi. Nilipambana kupitia ajenda nilizoandaa, nikazitumia vizuri kumpiga yule jamaa, tukashinda, tukaenda kule Kyerwa alikuwapo Mutungireyi.
“Nikafanya mkakati mzito wa kupata mgombea mzuri. Nilimleta Khamis Kagasheki, alikuwa anafanya kazi Geneva nchini Uswisi, ni mtu aliyekuwa mwenye uwezo. Aliniambia ataongoza kwa miaka mitano na hatataka kugombea tena. Baada ya miaka mitano, yaani mwaka 2007 sikuchua fomu, nikastaafu uongozi wa aina yoyote wa kupigiwa kura hadi sasa.
Kuhusu changamoto alizokutana nazo kisiasa, Ngeze anasema zilikuwa za kawaida, kwa sababu kuna wakati mwana siasa analazimika kupita kwenye tundu la sindano kutokana na wingi wa wagombea.
“Unapokwenda kugombea mnakuwa wengi mno, mnapambana, ukibahatika unashinda, ukiisha kuingia kama kiongozi unakuwa kama jalala. Moja, makofi mengi na sifa nyingi mno. Hauambiwi mambo mabaya. Nina mchango ambao nilitoa ndani ya chama changu, nilikuwa kijana msomi, mwenye digrii wakati ule.
“Mwalimu Nyerere alinipenda sana, Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine alinipenda sana, walinitumia sana katika masuala mbalimbali, nilijitahidi kufanya mambo kutokana na uwezo niliokuwa nao,” amesema.
“Niliamua kustaafu kwenye nafasi hizi nikiwa na umri wa miaka 64, nikarudi kufanya shughuli zangu binafsi. Maisha yangu hayakuwa kwenye siasa tu, serikali imenitumia sana, hasa marehemu Rais Ali Hassan Mwinyi wakati wa uhai wake,” amesema.
Amesema hayati Mwinyi alimteua kuwa mjumbe wa bodi mbalimbali 16. Pia aliwahi kuongoza Bodi ya Kahawa na Benki ya CRDB.
“Mimi ndiye mwanzilishi wa Benki ya CRDB, na kazi hii nilipewa na Rais Mwinyi – kubadili benki ya serikali iwe benki ya binafsi. Walionunua hisa za kwanza wataona pale kuna sahihi yangu,” amesema.
Kuhusu nini ambacho anajivunia ndani ya mkoa wake, Ngeze anasema yapo mambo ambayo leo hii yameacha alama ya kudumu.
“Yapo mambo mengi mno, naona hayaandikwi katika vyombo vya habari. Nilipoingia katika uongozi mkoa huu ulikuwa na makabila, udini (madhehebu mengi), kulikuwa na wenyeji wanaitwa Wanyamahanga au Washuti, likawa kama jina la udhalilishaji hivi. Nilipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa nikajikuta Mshuti amekuwa kiongozi, jina hili likaanza kufa polepole.
“Maana mliyemkataa ndiye amekuwa kiongozi wenu, basi jina hili likaishia pale. Mara nyingi huwa ninakwenda vijijini ninawatania kwamba mliwahi kutuambia sisi ni Washuti, wanacheka, sasa limekwisha. Nilikuta wenyeji wa hapa wanaitwa Butojera. Ukiwa kiongozi jaribu kuwaambia mambo mapya,” amesema.
Amesema ndani ya mji wa Bukoba kulikuwa na mambo mengi, hata mtu wa kabila la Waziba kuchaguliwa na Wahaya wenzake ilikuwa vigumu, jambo ambalo lilikuwa linaondoa umoja, amani na mshikamano kama jamii.
“Tulifanya kazi kubwa mno ya kurudisha umoja. Waziba wenyewe pia ni Wahaya, haya mambo yalikuwa yamepitwa na wakati. Mambo yakaenda vizuri na kuonekana sina ubaguzi kati ya Myoza na asiyekuwa Myoza, Mziba na asiyekuwa Mziba, nilikuwa katikati kama kiongozi. Leo hii ukizungumza Mziba alitengwa na Mhaya imebaki historia tu, kwa hiyo haya ni mafanikio makubwa mno.
“Nakumbuka Jimbo la Nkenge ambalo sasa ni Jimbo la Misenyi, tuliunda jimbo lile kwa mkakati. Tulisema huyo akigombea na kushinda mtu fulani hatuwezi kutoka, kama mmeamua mipaka iwe hapa usiku unapigiwa simu mmeamua vibaya, hamjasaidia huyu bwana… ulikuwa mpango fulani hivi, usipoondoa hivi vitu. Ndiyo tukaunda Karagwe, Muleba Kaskazini, Kusini nao wana mambo yao. Tumejitahidi kusawazisha haya mambo, hata Chato ilitokana na misingi hii hii, ilikuwa inaitwa Biharamulo Kusini na Kaskazini,” amesema.
Amesema moja ya kitu ambacho hatakisahau maishani mwake ni kuundwa kwa Mkoa wa Kagera na kupewa jina hilo.
“Kagera hatusemi, nina mchango wangu, ukienda hata kwenye vikao vya Hazina kulikuwa na mkoa mmoja unaojulikana una majina mawili, Ziwa Magharibi. Yaani ulikuwa ukiitwa mkoa tunakuwa wa mwisho, hiki kitu kilikuwa kinaniudhi kwa kweli. Baada ya vita ya Kagera ambayo tulishinda, mimi nikiwa mwenyekiti wa mkoa, nikasema hapa ndipo pa kubadilishia jina. Nikapeleka ajenda kwenye Kamati ya Siasa ya Mkoa wakati ule tukajadiliana, kisha hoja zetu zikapelekwa serikalini ambako mwisho wa siku wakapitisha, hii ilikuwa furaha kubwa mno kwetu.
“Baada ya hapo mawazo yetu yakapelekwa kwenye vikao vya juu serikalini, mwisho wa siku tukaambiwa Mkoa wa Ziwa Magharibi sasa utaitwa Kagera. Jina hili lilitokana na mto wetu, haya ni mafanikio makubwa kwangu ambayo niliyapata wakati wa uongozi wangu,” amesema.

