NAIBU Waziri wa Afya, Florence Samizi amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati za kuimarisha afya za mama wajawazito na watoto nchini ikiwemo kuongeza miundombinu ya huduma, kuimarisha huduma za dharura wakati wa kujifungua, pamoja na kuboresha huduma za watoto wachanga kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Dkt. Samizi aliyasema hayo juzi, bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe Esther Edwin Maleko kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa kuhusu mkakati wa Serikali wa kuimarisha huduma za afya kwa kina mama wajawazito na watoto.
Akifafanua hatua zinazochukuliwa, alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa kujenga vituo vya huduma za dharura kwa wajawazito na watoto wachanga (CEmONC), sambamba na kuanzisha wodi maalumu za watoto wachanga na wagonjwa ambapo hadi sasa jumla ya wodi 438 zimeanzishwa ikilinganishwa na wodi 14 pekee zilizokuwepo mwaka 2018.
Aidha, Serikali imeanza ujenzi wa vitengo maalumu vya huduma kwa watoto wachanga wanaohitaji uangalizi maalumu (NICU) 37 katika mikoa na halmashauri zenye idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa, hatua inayolenga kuboresha huduma na kuongeza nafasi ya watoto wachanga kuishi.
Dkt. Samizi amesema katika kuimarisha ubora wa huduma, Serikali imeendelea kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ambapo jumla ya wahudumu 18,929 wamepatiwa mafunzo ya huduma za upasuaji wa dharura, usimamizi wa vyumba vya upasuaji pamoja na utoaji wa dawa za usingizi tiba na ganzi salama.
Pia, Serikali iliendelea kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba kwa ajili ya huduma za watoto wachanga, wajawazito na kina mama baada ya kujifungua ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana katika vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini.
Sambamba na hilo, Dkt. Samizi alisema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kinga kwa kuhakikisha chanjo pamoja na vifaa vya kutolea chanjo vinapatikana muda wote kulingana na mahitaji, huku huduma za ukunga nazo zikiendelea kupewa msisitizo kupitia matumizi ya chati uchungu na maboresho ya vyumba vya kujifungulia ili kuwezesha huduma ya mwambata.


