Na Mwandishi Wetu, Mkuranga
UONGOZI wa Shule ya Awali na Msingi ya Courage iliyopo eneo la Kibamba wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani umekabidhi msaada wa chakula, mavazi na bidhaa mbalimbali kwa Kituo cha Watoto Yatima cha Lord’s Children Home kilichopo Kimanzicha wilayani humo.
Akizungumza kituoni hapo muda mfupi baada ya kukabidhi msaada huo, Meneja wa shule hiyo, Bi. Theodosia Lyimo amesema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa shule yake kusaidia jamii hasa zile ambazo hazijiwezi.
“Uongozi wa shule kwa kushirikiana na wafanyakazi pamoja na wanafunzi tumekuja hapa leo kwa ajili ya kutoa tabasamu kwa watoto hawa yatima na wenye mahitaji maalumu” alisema Bi. Lyimo.
Alisema wanatambua jamii nyingi zina changamoto mbalimbali lakini wameamua kwenda kituoni hapo kwa ajili ya kuwasaidia watoto kwani hao ndiyo taifa la kesho na muhimu kuchangia katika malezi na kutimiza ndoto zao.
Bi Lyimo alisema kuwa watoto hao kuishi hapo siyo kwa sababu walimkosea Mungu la-hasha, ni mipango yake katika kuwafikisha katika hatma ya maisha yao, hivyo wasichukiliwe kama ni wakosaji bali ni sehemu mojawapo ya makuzi.
“Tunaamini mavazi haya pamoja na chakula vitasaidia kwa kipindi hiki ambacho kituo kina upungufu wa chakula, na shule yetu itakuja mara kwa mara kutoa tabasamu kwa watoto ”, alisema.
Bi. Lyimo aliwaasa wanafunzi wa kituo hicho kuwaheshimu viongozi na walezi wao kipindi chote na kujiepusha na makundi maovu ya mtaani yasiyofaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo hicho,Bw Ezekiel Mabesa mbali ya kuushukuru uongozi wa Shule ya Courage kwa mkubwa kwa kituo chake,aliziomba taasisi na mashirika mbalimbali kuiga mfano wa Shule ya Courage.
“Kama shule tunajua ratiba yenu ni ngumu sana kupata nafasi ya kufanya jambo la kijamii nje ya shule, lakini kwa upendo na uthubutu wenu mmeweza kufanya hivyo”, alisema Bw Mabesa.
Alisema kituo chake kina watoto 33 wenye umri wa miaka miwili hadi 16 wa kiume na wa kike ambapo wanapa mahitaji yote ya msingi kama watoto wengine wanavyostahili.
“Tunaomba shule nyingine zije kutembelea watoto wetu hapa kituoni na kuwapa faraja,” alisema na kuongeza kuwa msaada umekuja wakati mwafaka.





