Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amewataka Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuitumia Sikukuu ya Eid El Adha kama fursa ya kuimarisha umoja, mshikamano na kudumisha amani ya taifa.
Ujumbe huo umetolewa leo Jumatano Mei 27, 2026 jijini Dodoma kupitia Msemaji Mkuu wa Mufti wa Tanzania, Dkt Harith Nkusa wakati wa ibada ya Eid, ambapo amesema Mufti amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira na kuishi kwa upendo ,ushirikiano na kuheshimiana ili kuendelea kuilinda Tanzania kuwa taifa lenye utulivu na mshikamano.
Dkt Nkusa amesema Eid Al Adha inapaswa kuwa kipindi cha kujikumbusha wajibu wa kila mwananchi katika kulinda amani, maadili ya jamii pamoja na mazingira yanayowazunguka wananchi.
“Mufti amewataka Watanzania kuitumia Eid hii kujikumbusha wajibu wa kulinda amani ya taifa letu, kutunza mazingira na kuepuka vitendo vya uchafuzi wa mazingira,” amesema Dkt Kusa.
Amesema Mufti pia amesisitiza kuwa amani huanzia katika ngazi ya familia, majirani, sehemu za kazi na jamii kwa ujumla kabla ya kujengwa taifa lenye mshikamano na utulivu wa kudumu.
Katika maelezo yake, Dkt Nkusa amesema Mufti ametolea mfano ibada ya Hija inayowakusanya mamilioni ya Waislamu kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa amani na mshikamano mkubwa bila migogoro, jambo linalodhihirisha umuhimu wa umoja na kuheshimiana miongoni mwa watu.
Aidha amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kuthamini taifa lao kwa kufuata sheria, maadili, misingi ya dini pamoja na sheria za nchi ili kuendelea kudumisha amani iliyopo.
“Mufti amesisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kulinda taifa lao kwa kufuata sheria, maadili na misingi ya dini kama ilivyoelekezwa katika Qur’an na Sunna pamoja na sheria za nchi,” amesema.
Naye mmoja wa waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Dodoma, Hamida Ramadhan amesema umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa na mafanikio ya jamii katika nyanja mbalimbali za maisha.
Amesema maendeleo ya taifa, jamii na hata familia hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa upendo, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wananchi.






