Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia ,Dodoma

Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu Shaaban amesema kutokuwepo kwa usikivu, utiifu na kuheshimu mamlaka katika jamii ni chanzo kikubwa cha migogoro, vurugu na uvunjifu wa amani, huku akiwataka wananchi kuendelea kutii viongozi na mamlaka halali ili kudumisha mshikamano wa Taifa.

Akizungumza katika ibada ya Eid El Hajj iliyofanyika leo Mei 27, 2026 katika Msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma, Sheikhe Shaaban amesema Waislamu wanapaswa kujifunza somo la utiifu kupitia historia ya Nabii Ibrahim na mwanawe Nabii Ismail, ambayo ndiyo msingi wa ibada ya kuchinja katika Sikukuu ya Eid El Adha.

Amesema makumi ya mwezi wa Dhulhijjah yamehitimishwa leo huku akiwaasa Waislamu wenye uwezo kutekeleza ibada ya kuchinja kama ilivyoelekezwa katika dini ya Kiislamu.
“Si hadithi ya kawaida, ni simulizi inayotufundisha utiifu na usikivu.

Nabii Ibrahim alimweleza mwanawe kuwa ameona katika ndoto anamchinja, jambo linalotufundisha namna ya kuheshimiana, kusikilizana na kutii mamlaka,” amesema Sheikhe Shaaban.

Amesema pale jamii inapokosa utamaduni wa kusikilizana na kuheshimu mamlaka ndipo migogoro, chuki na hata umwagaji damu hujitokeza, hali inayoweza kuhatarisha amani ya Taifa.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuendelea kuishi kwa upendo, amani na kuheshimiana ndani ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
Aidha, amesema dini ya Kiislamu inaelekeza waumini kuwatii Mwenyezi Mungu, Mtume Muhammad pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na kisiasa.

Sheikhe Shaaban pia amesisitiza umuhimu wa kuheshimu taasisi na vyombo vinavyoundwa kwa ajili ya kusimamia masuala ya jamii na dini, akitolea mfano tume na kamati zinazoundwa ndani ya taasisi za kidini kama BAKWATA.

Amesema jamii inapojenga utamaduni wa kuheshimu maamuzi ya viongozi na taasisi halali, Taifa linaendelea kuwa na utulivu, mshikamano na maendeleo endelevu.