Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Zaidi ya tani 1,017 za bangi zimekamatwa nchini katika kipindi cha mwaka 2025, huku serikali ikieleza kuwa operesheni kali dhidi ya mitandao ya usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya zimeanza kuzaa matunda.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kiwango hicho cha bangi kilichokamatwa kimepungua kwa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka 2024, ishara ambayo serikali imesema inaonyesha mafanikio ya mapambano yanayoendelea dhidi ya biashara hiyo haramu.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini Leo Mei 29,2026 Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi amesema bangi imeendelea kuwa dawa ya kulevya inayoongoza kukamatwa nchini licha ya juhudi kubwa za kuidhibiti.

Amesema mafanikio hayo yametokana na operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi, kuimarishwa kwa udhibiti mipakani pamoja na ongezeko la elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya.

“Bangi ndiyo dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa kiwango kikubwa zaidi mwaka 2025, lakini hatua tulizochukua zimepunguza kwa kiasi kikubwa usambazaji wake,” amesema Prof. Kabudi.

Aidha Serikali ilitangaza kufanikiwa kukamata tani 29.52 za dawa mpya ya kulevya aina ya Kratom iliyokuwa imeingizwa nchini ikiwa imefichwa kwa jina la mbolea.

Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, uchunguzi uliofanywa baadaye ulibaini kuwa mzigo huo ulikuwa ni dawa za kulevya zinazotokana na mmea unaojulikana kitaalamu kama Mitrogyna speciosa.

Mbali na bangi, serikali pia ilikamata tani 26.36 za mirungi, kiwango kilichoonyesha ongezeko la asilimia 42.88 ikilinganishwa na mwaka uliopita, hali inayotafsiriwa kuwa ni kuimarika kwa operesheni za ufuatiliaji na ukaguzi katika maeneo ya mipaka.

Katika kundi la dawa za kulevya za viwandani, amesema Serikali ilikamata kilogramu 907.18 za methamphetamine, kilogramu 672.23 za heroin, kilogramu 4.89 za cocaine pamoja na kiasi kingine cha dawa aina ya MDMA na MDA.

Taarifa hiyo pia imeonyesha kuwa mashauri 1,124 ya dawa za kulevya yalifunguliwa mahakamani mwaka huu huku kesi 1,373 zikihukumiwa na serikali kushinda mashauri 1,058.

Aidha, mali zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.3 zilizohusishwa na biashara ya dawa za kulevya zilitaifishwa na serikali kama sehemu ya mkakati wa kuvunja nguvu ya kifedha ya mitandao hiyo.

Prof. Kabudi amesema pamoja na operesheni hizo, serikali imeendelea kutoa huduma za tiba na utengamao kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya ambapo watu 85,425 walipata huduma katika vituo mbalimbali vya afya ya akili, kliniki za MAT na nyumba za upataji nafuu.

Hata hivyo, serikali imeonya kuwa biashara na matumizi ya dawa za kulevya bado ni tishio kubwa kwa ustawi wa jamii kutokana na kuendelea kuwaathiri vijana, kuchochea uhalifu na kuvuruga mfumo wa familia katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mapambano haya hayawezi kufanywa na serikali pekee. Ushirikiano wa wananchi, taasisi binafsi, wadau wa maendeleo na vyombo vya ulinzi ni muhimu ili kuifanya Tanzania kuwa salama dhidi ya dawa za kulevya,” alisema Prof. Kabudi.

Serikali sasa imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia, kufanya operesheni za pamoja na kuongeza uwezo wa taasisi zinazopambana na dawa za kulevya nchini.