Na Mwandishi Wetu,Jamhuri Media ,Dar es Salaam
Wachambuzi huru wa kisiasa wamewataka vijana kujiepusha na makundi yenye mienendo inayodaiwa kutokuwa na maslahi mema kwa taifa, wakisema kuwa baadhi ya vitendo vinavyofanywa kupitia mitandao ya kijamii vinaweza kuathiri sekta ya utalii na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 31, 2026, mchambuzi huru wa kisiasa Ahmedi Kombo alisema kuwa kuna vijana wanaodaiwa kutumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa au maudhui yanayoweza kuathiri taswira ya Tanzania, hali ambayo kwa mujibu wake inaweza kuathiri sekta ya utalii na mapato ya fedha za kigeni.
Kombo alisema sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia maendeleo ya nchi kupitia mapato yanayosaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu, huduma za maji, afya na umeme.
“Ninajisikia vibaya ninapoona sekta ya utalii ikitajwa au kuwasilishwa kwa namna inayoweza kuathiri taswira ya nchi. Utalii ni sekta muhimu inayochangia maendeleo na maisha ya wananchi wengi,” alisema Kombo.
Aidha, Kombo alidai kuwa licha ya changamoto hizo, Tanzania imeendelea kuvutia watalii, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuimarisha sekta hiyo.
‘Wananchi wanapaswa kutambua umuhimu wa kulinda sekta ya utalii kwa kuwa inagusa maisha ya watu wengi, wakiwemo madereva, waongoza watalii, wamiliki wa biashara ndogo na wafanyakazi wa sekta hiyo” alisema.
Pia alizitaka mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu watakaobainika kuvunja sheria au kuchochea taharuki kupitia njia mbalimbali za mawasiliano, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na mshikamano wa taifa.
Kwa upande wake, mwanaharakati huru Joseph Yona maarufu kama “Yona wa Chalinze” alisema Tanzania imeendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbalimbali katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, jambo ambalo kwa maoni yake limeongeza ushirikiano wa kimataifa na kuimarisha taswira ya nchi.
Yona alisema ujio wa viongozi mbalimbali wa mataifa nchini pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na utalii ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa mazingira ya nchi, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana katika kulinda amani, mshikamano na maendeleo ya taifa.
“Tuna wajibu wa kuendelea kuipenda nchi yetu, kulinda amani na kushiriki katika maendeleo ya taifa letu,” alisema.



