Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia Dar es Salaam

Shirika la Dunia la Haki Miliki, World
Intellectual Property Organization (WIPO) kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Nelson Mandela African Institution of Science and Technology wamezindua mradi wa miezi 12 unaolenga kutumia teknolojia zilizopo kwenye kanzidata za kimataifa za hakimiliki kuongeza thamani ya mazao.

Pia utalenga kupunguza gharama za uzalishaji wa kilimo na ufugaji nchini, hususan katika upatikanaji wa mbolea na chakula cha mifugo kwa gharama nafuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo Juni 1, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Amos Nungu, amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuchochea maendeleo ya uchumi, hasa katika sekta za kilimo na ufugaji.

Dk. Nungu amesema mradi huo unalenga kutambua, kuchambua na kuhamisha teknolojia ambazo muda wake wa ulinzi wa hakimiliki umeisha kupitia kanzidata za WIPO ili ziweze kufanyiwa maboresho kulingana na mazingira na mahitaji ya Tanzania kwa manufaa ya wakulima na wafugaji, sambamba na kuongeza thamani ya mazao.

“Mradi huu utajikita katika kutafuta teknolojia zinazofaa mazingira ya Tanzania kupitia kanzidata za WIPO, ambapo teknolojia hizo zitafanyiwa maboresho kulingana na mahitaji ya ndani na kutumika kuandaa mifano ya mashine na vifaa vitakavyosaidia kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa za kilimo,” amesema Dk. Nungu.

Ameeleza kuwa mradi huo utawezesha wataalamu na wabunifu wa ndani kupata teknolojia sahihi zitakazoboreshwa na kutumika katika uzalishaji wa chakula cha mifugo, uchakataji wa mazao pamoja na maendeleo ya viwanda vinavyotegemea malighafi za kilimo.

Kwa mujibu wa Dk. Nungu, utekelezaji wa mradi utaanza katika mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa, ukielekeza nguvu zaidi katika uzalishaji wa chakula cha mifugo kwa kutumia mabaki ya mazao ya kilimo, hatua inayotarajiwa kuongeza thamani ya mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea uwekezaji katika sekta ya kilimo na ufugaji nchini.

Aidha, amesema matumizi ya teknolojia hizo yatasaidia kupunguza utegemezi wa teknolojia ghali kutoka nje ya nchi, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza mchango wa ubunifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Loy Mhando, amesema mradi huo utasaidia kutumia taarifa zilizopo kwenye kanzidata za kimataifa za hakimiliki kutafuta teknolojia zinazoweza kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji, hasa katika uzalishaji wa chakula cha mifugo kwa kutumia mabaki ya mazao ya kilimo.

Amesema matumizi ya teknolojia hizo yatapunguza gharama za uzalishaji, kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Nchi Zenye Maendeleo Duni wa WIPO, Prevdovj Vaanching, amesema taasisi hiyo itaendelea kusaidia nchi zinazoendelea kutumia ubunifu na teknolojia kama nyenzo muhimu za kukuza uchumi na kufanikisha maendeleo endelevu.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Thomas Kivevele, amesema mradi huo utaimarisha uwezo wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti kuunganisha matokeo ya tafiti na mahitaji halisi ya soko ili kuongeza matumizi ya ubunifu katika uzalishaji wa bidhaa na huduma.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, mkulima na mfugaji kutoka Njombe, Anna Gombela, amesema wakulima na wafugaji wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za chakula cha mifugo pamoja na mbolea, hivyo mradi huo unatarajiwa kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kuinua kipato cha wananchi pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.