Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia ,Dodoma
Zaidi ya walimu 3,000 kutoka shule za awali, msingi na sekondari nchini wamejitosa katika mashindano ya kitaifa ya stadi za ufundishaji yanayolenga kuibua walimu wabunifu na kuimarisha ubora wa elimu nchini.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuwa Juni 6, 2026 itafanyika fainali ya Shindano la Nne la Kitaifa la Stadi za Ufundishaji kwa walimu wa shule za awali na msingi pamoja na shindano la pili kwa walimu wa shule za sekondari Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo June 2,2026 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema shindano hilo linalosimamiwa kwa ushirikiano kati ya Wizara na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji mashuleni.
Amesema jukwaa hilo linawapa walimu nafasi ya kuonesha uwezo wao wa kutumia mbinu za kisasa na shirikishi katika kufundisha, kupima maendeleo ya wanafunzi na kutoa mrejesho unaochochea ujifunzaji wenye matokeo bora.
“Shindano hili ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) unaolenga kuongeza umahiri wa walimu na kuboresha matokeo ya ujifunzaji kwa wanafunzi nchini,” amesema Wanu.
Ameeleza kuwa pamoja na kutambua walimu bora, mashindano hayo yanakusudia kuhamasisha matumizi ya mbinu zinazojenga stadi za karne ya 21, kuandaa maudhui ya kujifunzia yatakayowekwa kwenye Mfumo wa Kidijitali wa Ujifunzaji (LMS) na kuimarisha uwezo wa walimu katika ubunifu wa zana za kufundishia.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema walimu 3,153 walijisajili kushiriki mashindano hayo mwaka huu kupitia Mfumo wa National Teaching Skills Competition System (TSCS).
Hata hivyo, amesema walimu 1,263 pekee walikamilisha vigezo vya ushiriki kwa kuwasilisha video za ufundishaji pamoja na maandalio ya masomo yaliyohitajika kwa ajili ya tathmini.
Profesa Nombo amesema mashindano ya mwaka huu yamejikita katika maeneo saba muhimu ambayo ni kusoma kwa darasa la awali, Kiingereza kwa darasa la kwanza, ufaraguzi wa zana kwa darasa la pili pamoja na masomo ya Fizikia, Hisabati, Business Studies na Computer Science kwa shule za sekondari.
Amesema maeneo hayo yamechaguliwa kutokana na mchango wake katika kuimarisha stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), pamoja na kukuza stadi za ujasiriamali, lugha ya Kiingereza, sayansi, teknolojia na ubunifu kwa wanafunzi.
“Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Ufundishaji Bora, Taifa Imara’, ikionesha nafasi ya mwalimu katika kujenga kizazi chenye maarifa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa,” amesema Profesa Nombo.
Ameongeza kuwa mshindi wa kwanza katika kila eneo la ushindani atapata Sh milioni 2.5, kompyuta mpakato, cheti cha ushindi na cheti cha pongezi, huku shule anayofundisha ikipewa projekta kwa ajili ya kuimarisha mazingira ya ufundishaji.
Profesa Nombo amesema hatua nyingine muhimu ni kurekodi upya video za washindi wa kwanza katika studio za TET ili ziweze kupakiwa kwenye Mfumo wa Elimu wa Kidijitali (LMS) na kurushwa kupitia TET Soma Kwanza TV, hatua itakayowezesha walimu wengine nchini kujifunza na kunufaika na mbinu bora za ufundishaji.









