Na Mwavua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametoa tahadhari kwa wakurugenzi wa halmashauri mkoani humo kuacha kuwalea kwa kuwakumbatia watendaji wa vijiji na kata pamoja na viongozi wa chama wanaojihusisha na uchochezi wa migogoro ya ardhi kupitia uuzaji au ugawaji wa maeneo kiholela.
Aidha, amewaagiza wakurugenzi hao kutimiza wajibu wao kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu, ikiwemo kuwaondoa kazini watendaji watakaobainika kuhusika na migogoro ya ardhi.
Kunenge amesema iwapo atalazimika kuingilia kati na kutekeleza jukumu ambalo lilipaswa kufanywa na mkurugenzi husika, atafuata taratibu za kumwajibisha.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Biashara Mkoa wa Pwani kilichofanyika Juni 2, 2026, alisema amechoshwa na migogoro ya ardhi inayotokana na ukiukwaji wa makusudi wa taratibu katika ngazi za vijiji na kata.
Pia alikemea tabia ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya wawekezaji au watu wanaomiliki ardhi kihalali kwa lengo la kuishinikiza Serikali kuwapatia maeneo hayo.
“Tutabomoa nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria na tutatenda haki kwa kuzingatia maamuzi ya mahakama na vyombo vya sheria bila kumuonea mtu,” alisisitiza Kunenge.
Hata hivyo, alisema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kukuza shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira na kuinua pato la Taifa.
Alieleza kuwa Mkoa wa Pwani tayari umejipanga vizuri katika utekelezaji wa Dira ya 2050 katika sekta ya Biashara na uwekezaji kwa kuimarisha miundombinu wezeshi.
“Mkoa wetu unaendelea kufanya vizuri kitaifa katika sekta za biashara, uwekezaji na viwanda, hadi mwezi Mei 2026, TRA imevuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 162, huku mamlaka za serikali za mitaa zikikusanya zaidi ya shilingi bilioni 109,” alieleza Kunenge.
Kunenge alibainisha kuwa ,halmashauri za Mkoa wa Pwani zimeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, lakini akasisitiza kuwa Serikali haitaki kuona mapato yakikusanywa kwa mabavu.
Alizitaka mamlaka za serikali za mitaa kuiga utaratibu unaotumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi, kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza mapato ya serikali.





