Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP-Centre), David Kafulila ameahidi kufanya kila kinachowezekana kuhakikisha Chuo kikuu Cha Dodoma (UDOM) kinaanza kutoa shahada ya uzamili ya Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (Masters of Public-Private Partnership (PPP).

Akizungumza katika mhadhara wa umma ulioandaliwa na UDOM leo Jumatano (Juni 3, 2026) chuoni hapo, Kafulila amesema kuwa kuna nchi chache duniani zinazotoa programu hiyo huku akiitaja Malaysia kama miongoni mwa nchi zinazotambulika zaidi duniani kwa utoaji wa programu ya PPP.

Kafulila amesema kuanzishwa kwa programu hiyo kutasaidia kujenga wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika masuala ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, jambo litakalochangia maendeleo ya kiuchumi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini.

Aidha, ameeleza kuwa uwepo wa programu ya PPP chuoni hapo utaimarisha uwezo wa nchi kuzalisha wataalamu wa ndani watakaosaidia kusimamia na kuendeleza miradi ya ubia kwa ufanisi zaidi, sambamba na kukuza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa.