Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Licha ya kuwepo kwa mijadala inayoendelea ndani ya ulingo wa kisiasa
,Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imesisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kuwa imara na chenye mshikamano , ikieleza kuwa kauli za mtu mmoja mmoja haziwezi kubeba msimamo rasmi wa chama chenye wanachama zaidi ya milioni 13 nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo June 4,2026 jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya Wiki ya Wazazi itakayofikia kilele Julai 4, 2026 mkoani Mwanza, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Fadhili Mganya, amesema CCM imeendelea kubaki imara hata pale ambapo hutokea mitazamo tofauti kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanachama wake hadharani.

Amesema hali ya mijadala ya kisiasa inayojitokeza mara kwa mara, ikiwemo kauli zinazotolewa na baadhi ya wawakilishi katika vikao mbalimbali vya maamuzi, haipaswi kutafsiriwa kama msimamo wa chama kizima, bali ni mitazamo binafsi ya wahusika.

“Mtu mmoja hawezi kuwakilisha msimamo wa CCM. Chama chetu kina wanachama zaidi ya milioni 13 na kina taratibu zake za kutoa msimamo rasmi kupitia viongozi wake wa kitaifa,” amesema Mganya.

Kauli hiyo imekuja katika mazingira ya mjadala wa kisiasa ulioibuka kufuatia matamshi ya Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mohamed Simai Said, aliyoyatoa bungeni wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Fedha, jambo lililoibua tafsiri tofauti ndani ya jamii ya kisiasa.

Hata hivyo, Mganya amesema chama kinaendelea kusimama imara bila kuyumbishwa na mijadala hiyo, akisisitiza kuwa CCM ina mifumo madhubuti ya uongozi na maamuzi ambayo hulinda mshikamano wake wa ndani.

Amefafanua kuwa viongozi wenye mamlaka ya kutoa msimamo rasmi wa chama ni Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu Wenyeviti wa CCM Tanzania Bara na Zanzibar, Katibu Mkuu pamoja na Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo.

Wakati huohuo, Jumuiya ya Wazazi ya CCM imetangaza kuanza maandalizi ya waraka maalumu wa kuimarisha malezi na makuzi ya watoto kwa kuzingatia maadili, mila na desturi za Kitanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto za kijamii zinazoathiri kizazi kipya.

Mganya amesema mwongozo huo unalenga kusaidia jamii kurejea katika misingi ya malezi bora, huku akisisitiza kuwa malezi ni jukumu la jamii nzima na si la wazazi pekee.

Amesema kabla ya kilele cha Wiki ya Wazazi kutafanyika kongamano la kitaifa litakalowakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala ya malezi, maadili na ustawi wa jamii na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha makuzi ya watoto nchini.

Kwa mujibu wake, maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na maeneo matano muhimu ambayo ni elimu, malezi na maadili, mazingira, afya na utamaduni, huku shughuli mbalimbali zikitarajiwa kufanyika Tanzania Bara na Zanzibar kuhamasisha jamii kushiriki katika kujenga kizazi chenye maadili na uzalendo.