Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026,Amina Sanga ametangaza rasmi majina ya vijana 100 bora waliofanikiwa kuingia hatua inayofuata ya shindano hilo baada ya mchakato mkali ulioshirikisha jumla ya maombi 7,852 kutoka mikoa yote nchini Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari, Sanga June 4,2026 Kijijini hapa amesema shindano hilo linalenga kuibua mawazo bunifu ya vijana yatakayosaidia kuimarisha uchumi wa taifa katika kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi duniani, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameeleza kuwa mwitikio wa vijana ulikuwa mkubwa, ambapo sekta ya TEHAMA na huduma za kidigitali iliongoza kwa asilimia 30.7 ya mawazo yaliyowasilishwa, ikifuatiwa na kilimo na teknolojia za kilimo kwa asilimia 27.8, huku sekta ya viwanda na uzalishaji ikichangia asilimia 21.3.

Amesema baada ya uchambuzi wa awali, maombi 4,121 sawa na asilimia 52.5 yalitimiza vigezo vya msingi vya ushiriki, na kati ya hayo mawazo 458 yalipata alama za juu na kuingia hatua ya mwisho ya tathmini kabla ya kupatikana kwa washiriki 100 bora.

Amesema vijana hao 100 wamechaguliwa kutokana na ubora wa mawazo yao, kiwango cha ubunifu, uwezekano wa utekelezaji pamoja na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.

“Kufika katika hatua hii ni mafanikio makubwa kutokana na ushindani uliokuwepo. Kila mshiriki amebeba wazo lenye thamani kubwa kwa mustakabali wa uchumi wa nchi,” amesema Sanga.

Aidha, washiriki hao wataingia katika kambi maalum ya mafunzo ya siku nne, ambapo watapatiwa mafunzo ya kitaalamu, ushauri wa kuboresha mawazo yao na mbinu za uwasilishaji kabla ya hatua ya kuchuja kufikia washiriki 30 bora, na baadaye 10 bora watakaoingia fainali.

Sanga ameongeza kuwa kutokana na ubora wa mawazo yaliyowasilishwa mwaka huu, zawadi zimeongezwa ambapo mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 50, mshindi wa pili milioni 30, na mshindi wa tatu milioni 20.

Aidha, washiriki wote 100 bora watapatiwa vyeti vya utambuzi pamoja na fursa za mafunzo, ushauri wa kitaalamu na kuunganishwa na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kusaidia kuendeleza mawazo yao kwa manufaa ya taifa.