Aliyekuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amewataka wanasiasa nchini kujikita katika masuala ya maendeleo ya wananchi badala ya kuanza kampeni za kutafuta urais wa mwaka 2030 wakati ni miezi sita pekee tangu Serikali ya sasa iingie madarakani.
Doyo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga baada ya kuhitimisha ziara yake ya kisiasa katika mkoa huo ambapo alisema hali ya baadhi ya viongozi kuanza kuonyesha nia ya kugombea urais mapema ni ishara inayoweza kuathiri utekelezaji wa agenda za maendeleo na mijadala yenye tija kwa Taifa.
Alieleza kuwa, ingawa kila Mtanzania anayekidhi vigezo vya kisheria ana haki ya kuwania nafasi yoyote ya uongozi, jambo la kushangaza ni kuona baadhi ya wanasiasa kutoka chama tawala wakianza kuzungumzia urais wa mwaka 2030 katika kipindi kifupi baada ya uchaguzi mkuu kumalizika na Serikali mpya kuanza kazi.
“Ni miezi sita tu tangu Rais aapishwe na kuanza kutekeleza majukumu yake, Bado taifa lina safari ndefu katika awamu hii ya uongozi, lakini tayari kuna baadhi ya wanasiasa wanaotoa kauli zinazoashiria kutamani urais wa mwaka 2030. Hili si jambo lenye afya kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema Doyo.
Alibainisha kuwa jukumu kubwa la viongozi waliopewa dhamana na wananchi kwa sasa ni kuhakikisha wanasimamia sera, mipango na mijadala itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, badala ya kuelekeza nguvu katika harakati za kisiasa za uchaguzi ambao bado uko mbali.
Kwa mujibu wa Doyo, wabunge na viongozi wengine wa chama tawala wanapaswa kutumia nafasi walizonazo kuishauri na kuisimamia Serikali kupitia Bunge ili kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya maendeleo yanayotarajiwa, badala ya kutumia majukwaa ya mijadala ya kitaifa kutangaza nia ya kuwania urais.
Alisema hali ya viongozi kuibuka katika mijadala ya bajeti au masuala mengine muhimu ya kitaifa na kuanza kuzungumzia urais wa mwaka 2030 inaondoa umakini katika hoja za msingi zinazohusu maisha ya wananchi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
“Tunahitaji mijadala yenye afya inayolenga kutatua changamoto za wananchi. Kiongozi anapokuwa na mawazo ya urais muda wote, kuna hatari ya kupoteza mwelekeo wa kushughulikia matatizo ya msingi yanayowakabili Watanzania,” alisisitiza.
Doyo alitoa wito kwa wanasiasa wa vyama vyote nchini kutumia kipindi hiki kushirikiana katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo, badala ya kuingia katika ushindani wa kisiasa wa mapema ambao unaweza kuathiri umoja na mshikamano wa kitaifa.
Aidha, alisema viashiria vya baadhi ya viongozi kuanza kuwania urais kabla hata ya mwaka mmoja wa uongozi wa Rais wa sasa kukamilika vinaweza kuonyesha kuwepo kwa makundi yenye maslahi ya kisiasa ndani ya chama tawala, jambo ambalo linaweza kuathiri utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo.
Alionya kuwa endapo hali hiyo itaendelea, inaweza kuzorotesha usimamizi wa masuala muhimu ya maendeleo na kuhamisha mjadala wa taifa kutoka kwenye utatuzi wa changamoto za wananchi kwenda kwenye siasa za urithi wa madaraka.
Doyo aliwataka viongozi wa chama tawala kuelekeza nguvu zao katika kumsaidia Rais kutekeleza ahadi zake kwa wananchi na kuhakikisha huduma za kijamii, uchumi na maendeleo zinaboreshwa, huku akisisitiza kuwa wakati wa kuwania urais ukifika hakuna atakayezuiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
“Tunawaomba Watanzania kutambua kuwa kwa sasa taifa linahitaji viongozi wanaotatua kero za wananchi badala ya kujijengea mazingira ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi ujao. Kipaumbele kiwe maendeleo ya wananchi na si mbio za urais ambazo muda wake bado haujafika,” alisema.
Katika kikao hicho, MWenyekiti wa NLD wilaya ya Tanga Abdul Karney alieleza kuwa wananchi wa Mkoa wa Tanga bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara katika maeneo kadhaa pamoja na uhaba wa maji katika baadhi ya wilaya, hali inayohitaji juhudi za viongozi katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Kiongozi huyo alisema wananchi wanatarajia kuona viongozi wakisimamia masuala ya maendeleo na utatuzi wa kero zinazowagusa moja kwa moja, badala ya kujihusisha na mijadala ya urais wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika miaka kadhaa ijayo.
Alisisitiza kuwa maendeleo ya wananchi yanapaswa kuwa ajenda kuu ya viongozi wote kwa sasa, huku akitoa wito kwa wadau wa kisheria.

