Hatua madhubuti za ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo zilizochukuliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga zimezaa matokeo makubwa baada ya kuokoa zaidi ya Shilingi milioni 116 ambazo zilikuwa katika hatari ya kupotea, huku miradi muhimu ya elimu iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu ikirejea kwenye utekelezaji na kuanza kuwanufaisha wananchi.
Mafanikio hayo yameelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji, usimamizi wa fedha za umma na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali katika sekta ya elimu.
Akitoa taarifa ya utendaji wa TAKUKURU kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwata, alisema taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa Shilingi milioni 116.2 kupitia ufuatiliaji wa karibu wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo.
Alisema miongoni mwa miradi iliyonufaika na hatua hizo ni ujenzi wa madarasa mawili wenye thamani ya Shilingi milioni 53.8 pamoja na mradi wa ujenzi wa vyoo wenye thamani ya Shilingi milioni 40 katika Shule ya Sekondari Chongoleani.
Kwa mujibu wa Ndwata, miradi hiyo ilikuwa imekwama kwa muda licha ya fedha kutolewa tangu Machi 4, 2024 kutokana na changamoto za kiutendaji na manunuzi.
Alieleza kuwa makadirio ya gharama za vifaa vya ujenzi yaliandaliwa chini ya bei halisi za soko, hali iliyosababisha Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) kukataa zabuni zote zilizowasilishwa.
“Katika mradi wa vyoo tulibaini kuwa hakukuwa na maandalizi ya makadirio ya gharama za ujenzi, jambo lililosababisha taratibu za manunuzi kutokuanzishwa kabisa. Baada ya ushauri, usimamizi na hatua za uwajibikaji kuchukuliwa, utekelezaji wa miradi hiyo umeanza na unaendelea vizuri,” alisema Ndwata.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU imefanikiwa kufuatilia na kuchochea maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kwabastola iliyopo wilayani Muheza wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.06.
Ndwata alisema kupitia ufuatiliaji huo, kazi mbalimbali zilizokuwa zimekwama zimekamilishwa, ikiwemo upakaji varnish kwenye milango ya shule, marekebisho ya mikanda ya gypsum na ununuzi wa vitanda 57 vyenye thamani ya Shilingi milioni 22.4 kwa ajili ya wanafunzi.
Aliongeza kuwa TAKUKURU inaendelea kufuatilia hatua za mwisho za ukamilishaji wa mradi huo, zikiwemo kazi za sakafu, uwekaji wa vigae na ununuzi wa vitanda vingine 23 ili shule hiyo iweze kufanya kazi kwa ufanisi kamili.
“Awali vitanda 80 vilihamishwa na kupelekwa katika Shule ya Sekondari Muheza High kutokana na mradi kutokamilika kwa wakati. Sasa tunaendelea kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika ili miundombinu yote itumike kama ilivyokusudiwa,” alisema.
Katika kipindi hicho, TAKUKURU Mkoa wa Tanga ilifuatilia jumla ya miradi 49 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 506.7 inayotekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, barabara na utawala.
Mbali na ufuatiliaji wa miradi, taasisi hiyo imeendelea kuimarisha vita dhidi ya rushwa kwa kutoa elimu kwa wananchi kupitia njia mbalimbali za uhamasishaji. Ndwata alisema jumla ya wananchi 189,521 walifikiwa kupitia semina 57, mikutano ya hadhara 28, klabu 163 za wapinga rushwa, maonesho 10 pamoja na vipindi 37 vya redio.
Aidha, TAKUKURU ilipokea malalamiko 133 katika kipindi hicho ambapo malalamiko 100 yalihusu vitendo vya rushwa na mengine 33 hayakuhusu rushwa.
Alisema malalamiko yote yanayohusu rushwa yalifunguliwa majalada ya uchunguzi kwa ajili ya hatua za kisheria, huku yale ambayo hayakuhusu rushwa yakipelekwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kushughulikiwa.
Kwa upande wa mashauri ya mahakamani, Ndwata alisema mashauri mapya 11 yalifunguliwa katika kipindi hicho na kufanya jumla ya mashauri 18 ya rushwa kuendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali.
Akihitimisha taarifa yake, Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa fedha za umma na matumizi mabaya ya rasilimali za Serikali.
“Mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi. Tunapolinda fedha za umma, tunalinda maendeleo ya taifa letu. Kuzuia rushwa ni jukumu la kila mmoja wetu,” alisema.



