Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Kibaha

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewasihi wananchi wanaodaiwa kuvamia Shamba Na. 34 Mitamba, Kata ya Pangani, Manispaa ya Kibaha, kuacha mara moja shughuli zote za maendeleo katika eneo hilo na kusubiri maamuzi ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kuhusu mgogoro unaoendelea.

Akizungumza na baadhi ya wananchi waliofika katika eneo hilo Juni 8, 2026, Kunenge alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba migogoro lazima itatuliwe kwa kuzingatia taratibu, sheria za nchi na maamuzi ya mamlaka .

Alisema awali Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliunda timu ya uchunguzi iliyojumuisha wataalamu na vyombo vya dola ili kufuatilia kwa kina mgogoro huo.

“Baada ya uchunguzi kukamilika, timu hiyo ilifanya mkutano wa hadhara katika eneo husika ikiongozwa na Waziri wa Ardhi akiwa ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa wakati huo” ambapo uchunguzi ulibaini kuwa wananchi walivamia ardhi hiyo ya Serikali”

Kunenge aliongeza kuwa, pamoja na wahusika kufikisha malalamiko yao mahakamani na kwa viongozi mbalimbali wa juu wa chama na serikali, maamuzi yaliyotolewa yaliwataka kuondoka katika eneo hilo.

Hata hivyo, wananchi hao wametumia haki yao ya kikatiba kuwasilisha malalamiko yao kwa Waziri Mkuu, ambaye amewasikiliza, hivyo ni muhimu kusubiri uamuzi wake badala ya kuendelea na shughuli za ujenzi au maendeleo katika eneo hilo.

“Yeyote atakayevunja sheria atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, Hakuna atakayeonewa, lakini sheria lazima ifuatwe,” alisisitiza Kunenge.

Kadhalika Kunenge aliwataka wananchi, kutokubali kupotoshwa na watu wenye maslahi binafsi .

Amemuelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, kuhakikisha hakuna shughuli mpya za ujenzi, ugawaji au maendeleo yoyote yanayoendelea katika eneo hilo hadi maamuzi ya mwisho yatakapotolewa.

Taarifa zinaonyesha kuwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kupitia Wizara ya ardhi katika kipindi cha mwaka 2022/2023 ilitoa agizo la kuondoka kwa zaidi ya kaya 130 zilizokuwa zimevamia Shamba Na. 34 Mitamba, ambalo ni mali ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 4,000 sawa na ekari 10,000 lilitengwa kwa matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi huku wizara ikiwa imekubali kuipatia Halmashauri ya Mji wa Kibaha hekta 2,963 bila malipo yoyote na kubaki na hekta 1,037.