Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mfumo wa bandari za Tanzania umeingia katika hatua mpya ya ukuaji wa biashara baada ya takwimu za hivi karibuni kuonesha ongezeko kubwa la Shehena za magari, makontena na mizigo ya kichele inayopitishwa bandarini.

Ukuaji huo unaashiria kuongezeka kwa shughuli za biashara na kuibua hitaji la kuimarisha mifumo ya usafirishaji na ugavi ili kuhakikisha mizigo inafikishwa kwa haraka zaidi katika masoko ya ndani na ya kikanda.

Ukuaji mkubwa zaidi umeonekana katika mizigo ya aina ya RoRo (Roll-on/Roll-off), inayojumuisha Shehena ya magari ambapo idadi ya magari yaliyohudumiwa imeongezeka kutoka magari 16,177 mwezi Mei 2025 hadi 30,442 mwezi Mei 2026, sawa na ongezeko la asilimia 88 ndani ya mwaka mmoja. Hii ni ongezeko la magari 14,265 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita.

Sambamba na hilo, idadi ya meli za magari zilizowasili bandarini imeongezeka kutoka Meli 9 kwa mwezi Mei 2024 kufikia Meli 13 kwa mwezi Mei 2025 hadi Meli 20 za sasa kwa mwezi Mei 2026. Hali hii inaonesha kuongezeka kwa shughuli za usafirishaji wa Shehena za magari kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Katika upande wa makontena, kampuni ya DP World ambao ni waendeshaji wa bandari ya Dar ea Salaam kutoka gati namba 1 hadi 7, ilihudumia makontena 44,001 (TEUs) mwezi Mei 2026, kutoka makontena 27,953 mwezi Mei 2025, sawa na ongezeko la asilimia 57. Hii ni nyongeza ya makontena 16,048 ndani ya mwaka mmoja. Kutokea mwezi Mei 2024 ambapo makontena 13,779 yalihudumiwa na sasa kiasi hicho kimeongezeka kwa zaidi ya makontena 30,000.

Aidha, idadi ya meli za makontena zilizohudumiwa na DP World imeongezeka kutoka meli 13 mwezi Mei 2025 hadi meli 20 mwezi Mei 2026, ikilinganishwa na meli 7 tu za mwaka 2024.

Nayo Kampuni ya Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited ( TEAGTL ) waendeshaji wa gati namba 8 hadi 11 katika Bandari ya Dar ea Salaam, ilihudumia Makontena 85,243 ( TEUs) mwaka 2026, kutoka Makontena 84,127 ( TEUs) Mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 1 ikiwa pia ni nyongeza ya makontena 20,049 ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu mwaka 2024 ambapo makontena 65,194 yalihudumiwa ikiwa ni ongezeko la Asilimia 30.75.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa mfumo wa bandari za Tanzania unahudumia kiwango kikubwa zaidi cha biashara na sasa unaelekea katika hatua mpya ya kuboresha mnyororo mzima wa usafirishaji wa mizigo.

“Ukuaji wa mizigo ya RoRo, makontena na mizigo ya kichele unaonesha kuimarika kwa biashara kupitia bandari za Tanzania. Kipaumbele chetu sasa ni kuhakikisha ukuaji huu unaendana na kasi ya utoaji wa mizigo, usafirishaji wa uhakika na kuimarisha miunganisho na maeneo ya ndani ya nchi,” amesema Bw. Mbossa.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, ongezeko la makontena lina manufaa makubwa zaidi ya shughuli za bandarini pekee kwani kila kontena linaloongezeka huongeza mahitaji ya huduma za uwakala wa forodha, maghala, vituo vya kuhifadhi mizigo, usafirishaji wa malori, bima, huduma za kifedha na usambazaji wa bidhaa katika masoko mbalimbali.

Mizigo ya kichele (Dry Bulk Cargo) nayo imeendelea kukua kwa kasi ambapo kiasi kilichohudumiwa kimeongezeka kutoka tani za metriki 210,488 mwaka 2025 hadi tani 267,560 mwaka 2026, sawa na ongezeko la asilimia 27. Ikilinganishwa na tani 86,318 zilizohudumiwa mwaka 2024, kiwango cha sasa ni kikubwa zaidi kwa tani 181,242.

Idadi ya meli za mizigo ya kichele pia imeongezeka kutoka meli 6 mwaka 2025 hadi meli 8 mwaka 2026, ikilinganishwa na meli 3 mwaka 2024. Hii inaongeza umuhimu wa uwekezaji katika vifaa vya kushughulikia mizigo, maeneo ya kuhifadhi na mifumo ya usafirishaji kwenda maeneo mbalimbali ya matumizi.

Ingawa mizigo mchanganyiko (General Cargo) imepungua kwa asilimia mbili kutoka tani 210,079 mwaka 2025 hadi tani 204,978 mwaka 2026, kiwango hicho bado ni kikubwa zaidi kuliko tani 113,699 zilizorekodiwa mwaka 2024.

Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa ukuaji mkubwa zaidi unatokana na magari, makontena na mizigo mikavu. Hali hiyo inaweka msingi mpya wa ukuaji wa sekta ya usafirishaji na ugavi nchini, huku fursa zikionekana zaidi katika usafiri wa barabara na reli, maghala, vituo vya ndani vya mizigo, mifumo ya kidijitali ya biashara, bima na huduma za usambazaji.

Kwa ujumla, bandari za Tanzania hususani Bandari ya Dar es Salaam imehudumia magari mengi zaidi, makontena mengi zaidi, mizigo ya kichele mingi zaidi na meli nyingi zaidi kuliko kipindi kama hicho mwaka uliopita. Changamoto na fursa iliyopo sasa si tu kuongeza kiwango cha mizigo, bali kuhakikisha mizigo hiyo inasafirishwa kwa haraka, kwa ufanisi na kwa manufaa makubwa zaidi kwa uchumi wa taifa.