Calgary, Canada

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Felchesmi Mramba, ameendelea kuitangaza Tanzania kimataifa kwa lengo la kuvutia uwekezaji zaidi katika Sekta ya Nishati akieleza kuwa Tanzania ni kitovu cha uwekezaji wa nishati barani Afrika.

Mramba amesema hayo wakati wa Mkutano wa Dunia wa Nishati ya Jotoardhi (World Geothermal Congress – WGC 2026) unaoendelea Calgary nchini Canada.

Amesema Tanzania ni kiungo muhimu katika biashara ya umeme kikanda kupitia ushiriki wake katika masoko ya umeme ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAPP) na Kusini mwa Afrika (SAPP), jambo linalotoa fursa kwa wawekezaji kufikia masoko mengi nje ya mipaka ya nchi.

Katika mkutano huo Mha.Mramba amewasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, akibainisha kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha miundombinu ya nishati ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme linalochochewa na ukuaji wa viwanda, shughuli za uchimbaji madini, sekta nyingine za kiuchumi na matumizi ya mwananchi mmoja mmoja.

Kuhusu nishati ya jotoardhi Mha. Mramba amebainisha kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya nishati hiyo kutokana na uwepo wake ndani ya Ukanda wa Ufa wa Afrika Mashariki, wenye uwezo kuzalisha zaidi ya megawati 5,000 za umeme.

Amesema pamoja na Serikali kuendelea na juhudi za kuendeleza miradi ya jotoardhi, inakaribisha ushiriki wa wawekezaji katika utafutaji, uendelezaji na matumizi ya rasilimali hiyo.

Aidha, amewahamasisha wawekezaji wa Canada kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya sekta ya nishati ikiwemo jotoardhi, gesi asilia, nishati ya jua, mifumo ya kuhifadhi nishati pamoja na maendeleo ya miundombinu ya umeme.

Kwa upande mwingine, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Canada katika mafunzo ya wataalam, uhamishaji wa teknolojia na uwekezaji wa pamoja katika miradi ya nishati safi na endelevu.

Mkutano huo wa Kimataifa wa Jotoardhi ni sehemu pia ya jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji kati ya Canada na nchi za Afrika, hususan katika sekta ya nishati, kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa nishati safi, ya uhakika na endelevu.