Na Mwavua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

Vikundi 51 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani, vimenufaika na mikopo yenye thamani ya Sh milioni 991.54 kupitia asilimia 10 ya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Vikundi hivyo vinaweka jumla ya vikundi 2,273 ambavyo tayari vimenufaika na mikopo hiyo katika Manispaa hiyo kwa kipindi hicho.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, aliielekeza Manispaa ya Kibaha kuhakikisha wajasiriamali wanaopata mikopo hiyo wanapatiwa mafunzo yatakayowasaidia kukuza na kuendeleza biashara zao.

“Hakuna biashara ndogo, Msikatishwe tamaa na maneno ya watu, Fanyeni kazi kwa bidii, muwe wabunifu na muendelee kupanua biashara zenu ili siku moja muwe wafanyabiashara wakubwa,” aliwasihi Koka.

Pia alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa mitaji kwa wananchi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani, hatua ambayo imepunguza utegemezi wa mikopo yenye riba kubwa kutoka taasisi za kifedha.

“Leo tunashuhudia jinsi mpango huu unavyoendelea kuleta tija kwa makundi maalum na kuinua maisha yao kiuchumi,” aliongeza Koka.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alieleza kati ya Sh milioni 991.54 zilizotolewa, Sh milioni 359 zimetengwa kwa vikundi 17 vya wanawake, Sh milioni 557.04 kwa vikundi 25 vya vijana na Sh milioni 75.5 kwa vikundi vya watu wenye ulemavu.

Dkt. Shemwelekwa alifafanua kuwa miradi iliyokopeshwa kwa vikundi hivyo ni usafirishaji, ambapo pikipiki 25, gari moja aina ya Toyota na bajaji nne zimenunuliwa, ufugaji wa kuku, uchomeleaji, ushonaji, utengenezaji wa batiki, sabuni na kilimo cha umwagiliaji.

Kwa upande wake, mnufaika wa mikopo hiyo kutoka kundi la watu wenye ulemavu, Amos Mhongole, alibainisha awali kikundi chao kilipatiwa Sh milioni 46 na kutokana na urejeshaji mzuri wa mkopo huo, wameongezewa mtaji.

Kadhalika aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira yanayowainua wajasiriamali wadogo na kuwawezesha kupanua shughuli zao za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Manispaa ya Kibaha, bajeti ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa makundi maalum katika mwaka wa fedha 2025/2026 ni Sh bilioni 1.099, fedha za marejesho ya mikopo zinatarajiwa kufikia zaidi ya Sh bilioni 1.9, huku bakaa ya miaka ya fedha 2022/2023 na 2023/2024 ikiwa Sh bilioni 1.1 na Sh milioni 632.9 , na kufanya jumla ya fedha kwa utoaji wa mikopo kufikia Sh bilioni 4.805.