Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF)Fortunatus Makore Magambo, amewataka Wabunge nchini kuwa mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa Tanzania kwa kuzitumia na kuzitangaza, ili kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa taifa.

Akizungumza leo Juni 15, 2026 katika Ukumbi wa Msekwa Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli na mafanikio ya Kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited (KLICL), Magambo amesema Tanzania ina rasilimali za kutosha na uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa bora za ngozi zinazoweza kushindana kikanda na kimataifa.

Amesema uwekezaji uliofanyika katika sekta ya ngozi umeiwezesha nchi kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kujenga msingi wa viwanda vinavyoweza kuhimili ushindani wa soko la dunia.

Kuhusu KLICL, Magambo amesema kiwanda hicho kimeendelea kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa vya uchakataji wa ngozi nchini, kikizalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo viatu, mikanda, mabegi na bidhaa nyingine zinazokidhi viwango vya ubora vya kimataifa.

“Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge muwe mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa hapa nchini. Mkitumia na kuzitangaza mtasaidia kujenga imani kwa wananchi na kuongeza soko la bidhaa zetu za ndani,” amesema Magambo.

Ameongeza kuwa ongezeko la matumizi ya bidhaa za ndani litasaidia moja kwa moja kuongeza thamani ya sekta ya mifugo, kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira kwa vijana na pia kuimarisha mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya nje.

Kwa mujibu wake, KLICL inaendelea kutekeleza mkakati wa kupanua masoko ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha uwezo wa uzalishaji uliowekezwa unatumika kikamilifu, huku masoko lengwa yakitajwa kuwa nchi za Afrika Mashariki, China, Saudi Arabia, Italia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Misri, Pakistan na Uturuki.

Katika hatua inayoonyesha kuimarika kwa ushindani wa bidhaa za ngozi za Tanzania kimataifa, menejimenti ya KLICL imeeleza kuwa wanunuzi kutoka China tayari wameidhinisha sampuli za bidhaa zake, hatua inayofungua milango ya oda kubwa zaidi katika siku zijazo.

Aidha, kiwanda hicho kimefanikiwa kuuza vipande 48 vya ngozi ya mbuzi kwenda China kwa thamani ya Dola za Marekani 15,000, ishara ya mwanzo ya kukua kwa soko la bidhaa hizo nje ya nchi.

Hata hivyo, Magambo amesema changamoto kubwa iliyopo ni upanuzi wa masoko kuendana na uwezo wa uzalishaji wa kiwanda hicho, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani.

Kwa ujumla, KLICL kinaendelea kujidhihirisha kama miongoni mwa viwanda vya kisasa zaidi vya uchakataji wa ngozi katika Afrika Mashariki na Kati, kikichochea ajenda ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda kupitia ongezeko la thamani ya rasilimali za ndani.