Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeishauri mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) masaa ya ziada irekebishe mara moja mapungufu yote yaliyoainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, katika ukusanyaji na usimamizi wa kodi.
Maelekezo hayo yametolewa wakati wa kikao maalumu cha PAC kilichoongozwa na Mwenyekiti wake Mbunge Devotha Minja, kilichokutana na uongozi wa juu wa TRA kupokea na kuchambua hesabu za mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025.
Minja amesisitiza kuwa ufanisi wa ukusanyaji wa kodi ni msingi muhimu wa kuimarisha mapato ya ndani na kupeleka maendeleo kwa wananchi. Hivyo imeitaka TRA kushughulikia kwa haraka dosari zote zilizobainishwa na CAG, hasa katika maeneo ya ukusanyaji wa kodi na usimamizi wa mapato ya serikali.
“Fedha zinazostahili kuingia hazipaswi kupotea. TRA inatakiwa kuimarisha mifumo yake, kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa walipakodi, kufanya uhakiki wa taarifa na kuboresha ufuatiliaji wa mapato ili kuongeza uwazi na tija,”amesema
Kwa upande wa Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema mamlaka hiyo imepokea maelekezo yote ya PAC kwa mikono miwili na tayari imejipanga kuyatekeleza kwa wakati ili kuboresha utendaji.
“Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali kuhakikisha changamoto zilizobainishwa zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu na kuongeza ufanisi wa huduma kwa walipakodi,” amesema Mwenda.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Uledi Mussa, amesema kikao hicho kimekuwa darasa kubwa la kujitathmini na kubaini maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu ili kuifanya TRA kuwa taasisi yenye ufanisi na inayoaminiwa zaidi.
Amesisitiza kuwa pamoja na kuimarisha mifumo ya ndani, TRA itaendelea kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari kama njia endelevu ya kuongeza mapato ya ndani na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ameiomba Kamati ya PAC kuendelea kuwa mshirika wa TRA katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari. “Ushiriki wa kila mdau ni nguzo muhimu katika kujenga uchumi imara na kuongeza uwezo wa serikali kugharamia huduma za kijamii,” amebainisha Uledi Mussa.





