Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Awamu ya Pili wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia utakaofanyika Juni 20, 2026 katika Viwanja vya Dole, Zanzibar, ikiwa ni mwendelezo wa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati kupitia huduma za msaada wa kisheria.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya uzinduzi huo leo June 17,2026 Jijini Dodoma ,Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Homera amesema kampeni hiyo ni utekelezaji wa maono na fikra za Rais Samia katika kuhakikisha wananchi wanapatiwa haki kupitia huduma za msaada wa kisheria katika mazingira mbalimbali yanayowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Amesema kampeni hiyo inashughulikia masuala mbalimbali ya kisheria ikiwemo madai ya kiraia, migogoro ya ardhi, mirathi, talaka, ndoa, haki za watoto, haki za wafanyakazi, ukatili wa kijinsia, uhalifu wa mtandao, masuala ya elimu, rushwa pamoja na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ikiwemo usuluhishi na mashauriano.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, programu hiyo imepewa jina la Rais Samia kwa kuwa ndiye kinara wa haki ambaye alibaini kuwa wananchi wengi walikuwa wanakosa haki zao kutokana na kutofahamu sheria, huku wengine wakichelewa kupata haki kutokana na ukosefu wa msaada wa kisheria.
“Rais Samia aliona wananchi wengi hawapati haki zao kwa wakati na wengine wanazikosa kabisa kwa sababu hawazijui sheria ndipo akaagiza Wizara ya Katiba na Sheria kuanzisha kampeni hii ili kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwasaidia kupata haki zao,” amesema.
Dkt.Homera amesema katika Awamu ya Kwanza ya kampeni hiyo, zaidi ya wananchi milioni nne wa Tanzania Bara walifikiwa na kupatiwa huduma za msaada wa kisheria, huku wengine wakisaidiwa kupata mawakili waliowasimamia katika mashauri yao hadi haki ikapatikana.
“Mheshimiwa Rais ameridhishwa na mafanikio yaliyopatikana katika awamu ya kwanza na sasa ameona twende awamu ya pili hadi Zanzibar,” amesema.
Amesema lengo la kupeleka kampeni hiyo Zanzibar ni kuendelea kuimarisha Muungano wa Tanzania kwa kuwa huduma ya msaada wa kisheria haibagui na inapaswa kuwafikia wananchi wote wa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Baada ya uzinduzi Zanzibar, huduma hizi zitaendelea kutolewa katika kanda zote, mikoa yote na vijiji mbalimbali nchini,tunaanzia Zanzibar kama sehemu ya kuimarisha umoja wetu na kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika kupata haki,” amesema.
Waziri huyo amesema maandalizi ya uzinduzi huo yamefanyika kwa zaidi ya mwezi mmoja na kwamba zaidi ya wananchi 20,000 wanatarajiwa kushiriki katika tukio hilo.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wananchi, amesema migogoro ya ndoa bado ni tatizo kubwa ambapo baadhi ya watu wanaendelea kukumbana na unyanyasaji wa kijinsia ndani ya familia.
Ametoa mfano wa tukio lililotokea mkoani Simiyu ambapo mwanamke mmoja alikuwa akifungiwa ndani na kupigwa na mume wake kabla ya mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtuhumiwa.
“Ukipigwa au ukinyanyaswa usikae kimya,sema ili hatua zichukuliwe,Sio wanawake pekee wanaonyanyaswa, hata wanaume wananyanyaswa,haki zilizopotea lazima zirejeshwe kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Amesema pia migogoro ya mirathi na talaka inaendelea kuwaumiza wananchi wengi, hivyo kampeni hiyo inalenga kutoa elimu ya sheria, ushauri wa kisheria na kuwasaidia wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto zao.
“Safari hii tunaenda kusambaza upendo katika jamii, kuwaelimisha wananchi na kuwapa tabasamu litakalosaidia kujenga jamii yenye amani, usawa na maendeleo,” amesema.
Kuhusu haki za wafanyakazi, Waziri amesema Serikali imekuwa ikishuhudia baadhi ya wafanyakazi wakidai madai yao kwa muda mrefu bila kulipwa, hali inayosababisha malalamiko mengi.
“Tutakwenda hadi katika ofisi za umma na taasisi mbalimbali kusikiliza changamoto hizo na kusaidia kuhakikisha haki za wafanyakazi zinapatikana kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Aidha, amesema wanafunzi pia ni miongoni mwa makundi yanayonufaika na kampeni hiyo kutokana na kuwepo kwa malalamiko ya kupewa adhabu au hatua za kinidhamu kwa makosa ambayo hawakuyatenda, huku wengine wakikumbana na changamoto za upangaji wa kozi.
“Tumeshughulikia changamoto nyingi za wanafunzi na tutaendelea kufanya hivyo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo zile zinazopambana na rushwa ili kuhakikisha haki inapatikana,” amesema.
Katika kukabiliana na vitendo vya rushwa, Waziri huyo amesema baadhi ya migogoro itatatuliwa kwa kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro ikiwemo usuluhishi na mashauriano ili kupunguza migogoro na kuharakisha upatikanaji wa haki.
Pia amesema kampeni hiyo itatoa elimu na msaada wa kisheria kuhusu uhalifu wa mtandao pamoja na mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.
“Sisi si mahakama. Sisi ni washauri wa kisheria. Tunawashauri wananchi kufuata sheria na taratibu ili haki ipatikane kwa mujibu wa sheria za nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa timu za kampeni hiyo zitafika hadi magerezani kusikiliza changamoto za wafungwa na mahabusu, ikiwemo wale wanaodai kubambikiziwa kesi au kukosa msaada wa kisheria.
Akihitimisha, Waziri huyo amesema uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni hatua kubwa ya kuondoa kero na changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi.
Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Amani na Maendeleo.”
“Tunaamini popote penye haki na usawa kuna maendeleo. Sheria ni maisha yako; kila hatua unayopitia inaongozwa na sheria. Hivyo kila Mtanzania anapaswa kufahamu haki zake na kutimiza wajibu wake,” amesema.


