Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (IAE) imesema imeendelea kuwa mhimili muhimu katika kupunguza ujinga, kuongeza ujuzi na kurejesha fursa za elimu kwa maelfu ya watoto, vijana na watu wazima waliokosa au kuacha masomo katika mfumo rasmi wa elimu nchini.
Akizungumza wakati wa maonesho ya Wiki ya Utumishi inayoendelea Dodoma , Mkuu wa Taasisi hiyo Prof.Philipo Sanga amesema IAE, ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miaka 51, ilianzishwa kwa lengo la kushughulikia mahitaji ya elimu kwa wananchi walio nje ya mfumo rasmi wa elimu na kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya kujifunza bila kujali umri wake.
Amefafanua kuwa dhana ya elimu ya watu wazima haimaanishi wazee pekee, bali inahusisha vijana na watu wazima wote ambao kwa sababu mbalimbali walikosa fursa ya kuanza shule, kuendelea na masomo au kukamilisha elimu yao katika mfumo wa kawaida.
“Katika jamii yetu bado kuna watoto na vijana wengi wanaokosa fursa za elimu kutokana na changamoto mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kimazingira. Wapo walioanza shule na kuacha njiani, na wapo ambao hawakupata kabisa nafasi ya kuanza masomo katika umri unaotakiwa,
Hili ndilo kundi ambalo taasisi yetu inalihudumia kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Ameeleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa bado idadi kubwa ya watoto wa umri wa kwenda shule hukosa kujiunga na elimu kwa wakati, huku wengine wakikatisha masomo kabla ya kufikia hatua za juu za elimu.
Aidha, amesema mamia ya maelfu ya wanafunzi huondoka katika mfumo wa elimu kila mwaka katika ngazi za msingi na sekondari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo changamoto za kifamilia, umbali wa shule, mimba za utotoni, ndoa za mapema na hali ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo, IAE imejikita katika kutoa elimu ya msingi na sekondari nje ya mfumo rasmi kupitia njia mbadala zinazowapa wanafunzi nafasi ya kurejea katika safari yao ya elimu bila vikwazo vya mfumo wa kawaida.
Amesema taasisi hiyo inasimamia programu mbalimbali za elimu mbadala zinazowawezesha wanafunzi waliokatisha masomo kurejea darasani, kufanya mitihani ya taifa na kupata sifa zinazotambulika rasmi kama wanafunzi wengine.
“Tunatoa elimu inayolenga kujenga maarifa, stadi za maisha na ujuzi unaomwezesha mwanafunzi kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” ameeleza.
Mbali na elimu ya msingi na sekondari, amesema taasisi hiyo pia ni chuo cha elimu ya juu kinachotoa mafunzo katika ngazi mbalimbali ikiwemo stashahada, shahada na shahada za uzamili kwa lengo la kuzalisha wataalamu watakaosaidia kuendeleza sekta ya elimu nchini.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo huandikisha zaidi ya wanafunzi 6,000 kila mwaka katika programu zake mbalimbali za elimu na mafunzo, hatua inayodhihirisha mahitaji makubwa ya elimu nje ya mfumo rasmi nchini.
Katika maonesho hayo, IAE imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo pamoja na mchango wake katika kupanua fursa za elimu kwa wananchi wa makundi yote.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kusisitiza falsafa ya kutomwacha mtu nyuma katika upatikanaji wa elimu, jambo ambalo limeiwezesha taasisi hiyo kuandaa mitaala nyumbufu inayokidhi mahitaji ya wanafunzi wenye mazingira tofauti.
Amefafanua kuwa maboresho mbalimbali yamefanyika katika programu za elimu mbadala kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na kuwafanya wanafunzi wanaosoma kupitia mfumo huo kufanya mitihani inayotambulika kitaifa na kupata matokeo yanayolingana na viwango vya mfumo rasmi wa elimu.
Kuhusu usimamizi wa shule huria, amesema IAE ndiyo mamlaka inayosajili shule hizo na kutoa mwongozo wa uendeshaji wake ili kuhakikisha zinazingatia viwango vya elimu vilivyowekwa.
Ameeleza kuwa mtu au taasisi inayotaka kuanzisha shule huria inapaswa kuwasilisha maombi rasmi kwa IAE, ambapo wataalamu wa taasisi hiyo hufanya ukaguzi wa miundombinu na mazingira ya kujifunzia ikiwemo madarasa, madawati, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na mahitaji mengine muhimu kabla ya kutoa usajili.
Aidha, amewataka wamiliki wa shule huria kuwekeza katika miundombinu bora ya elimu hususan maabara za sayansi ili kuwapatia wanafunzi mazingira yanayowawezesha kupata elimu yenye ubora na inayokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa.
“Ubora wa elimu hauwezi kupatikana bila uwekezaji katika mazingira bora ya kujifunzia,tunashauri shule huria zote kuhakikisha zinakuwa na maabara za kisasa, vifaa vya kujifunzia na walimu wenye sifa ili kuongeza ufaulu na ufanisi wa wanafunzi,” amesema.
Amesisitiza kuwa elimu nje ya mfumo rasmi imeendelea kuwa suluhisho muhimu kwa maelfu ya Watanzania waliokosa fursa ya kusoma kwa wakati, huku IAE ikiendelea kupanua huduma zake ili kuhakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kujifunza na kujenga maisha bora kupitia elimu.



