Na Mvuda Jaffer, WAF-Dar es Salaam

Wizara ya Afya imewataka waandishi wa habari na wadau wa mitandao ya kijamii kuendelea kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kutoka katika vyanzo rasmi ili kuimarisha uelewa wa wananchi na kuimarisha utayari wa taifa dhidi ya ugonjwa wa Ebola na dharura nyingine za afya ya umma.

Wito huo umetolewa leo Juni 30, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya, Dkt. Rahma Hingora wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na wadau wa mitandao ya kijamii kuhusu mawasiliano ya afya ya umma na utoaji wa taarifa sahihi ili kuimarisha utayari dhidi ya Magonjwa ya mlipuko ikiwepo Ebola.

“Serikali inawatambua waandishi wa habari kama wadau wa kimkakati katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi za afya kwa wakati, akisisitiza kuwa taarifa sahihi husaidia kujenga uelewa, kuondoa hofu na uvumi, kuimarisha imani ya wananchi kwa mamlaka za afya na kuwahamasisha kuchukua hatua stahiki za kujikinga,” amesema Dkt. Hingora

Dkt. Hingora amerudia kauli ya Serikali iliyotoewa hivi karibuni kuwa kwa sasa Tanzania haina mlipuko wa ugonjwa wa Ebola wala mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo, huku akieleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha utayari wa taifa kutokana na mwenendo wa ugonjwa huo katika baadhi ya nchi za ukanda wa Afrika.

Dkt.Hingora amefafanua kuwa, mafanikio ya jitihada hizo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, vyombo vya habari na wadau wa mitandao ya kijamii katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa zinazozingatia ushahidi wa kisayansi na taarifa rasmi zinazotolewa na Wizara ya Afya.

Dkt. Hingora amesema semina hiyo imelenga kuwajengea washiriki uelewa kuhusu hali ya utayari wa Tanzania dhidi ya Ebola, kuongeza uwezo wao wa kuwasilisha taarifa za afya kwa usahihi na kuwawezesha kupambana na taarifa potofu zinazoweza kuleta hofu kwa jamii.

“Kalamu, Kamera, Vipaza sauti na majukwaa ya kidijitali vina nafasi kubwa ya kuelimisha jamii na kulinda afya ya wananchi pale vinapotumika kusambaza taarifa sahihi.”amesema Dkt.Hingora

Katika hatua nyingine, Dkt. Hingora ameishukuru UNICEF kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mawasiliano ya afya ya umma, ushirikishwaji wa jamii na utayari dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Hingora amesema Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana kwa karibu na waandishi wa habari na wadau wa mitandao ya kijamii ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu masuala ya afya.