Dar es Salaam
Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Hassan Mussa Omar ameielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha inaongeza makusanyo ya kodi ili kuendana na hali ya ukuaji wa uchumi unaoendelea kushuhudiwa nchini.
Amezungumza hayo wakati akitembelea banda la TRA ndani ya Maonyesho ya Biashara ya 50 ya Kimataifa (Sabasaba) na kusisitiza kuwa TRA inapaswa kuonyesha ongezeko la makusanyo ya kodi ili kuakisi kiwango cha ukuaji wa uchumi.
“Serikali imeedelea kutekeleza mipango inayoimarisha hali ya uchumi na hivyo TRA inapaswa kuongeza ubunifu katika makusanyo ya kodi ili kuendana na hali ya ukuaji wa uchumi hivi sasa,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Aidha, amepongeza ushirikishwaji wa vilabu vya kodi ndani ya maonyesho na kuwaasa wanafunzi wa vilabu hivyo kuhakikisha wanafikisha elimu ya kodi kwa jamii ikiwemo kuhamasisha jamii kutokukwepa kodi kwa maendeleo ya nchi.
Maonyesho ya 50 ya Sabasaba yanafanyika ndani ya viwanja vya sabasaba jijini Dar es salaam na TRA imeshiriki ili kutoa huduma za kodi ikiwemo ushauri na elimu juu ya masuala mbalimbali yanayohusu kodi.









