Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katika hatua ya kuendelea kuimarisha usalama wa shughuli za kibandari na kulinda shehena za wateja, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imenunua boti mbili za kisasa za doria ziendazo kwa kasi, zenye thamani ya dola za Marekani 6,445,000, zitakazotumika katika Bandari ya Dar es Salaam na Bandari za Ziwa Victoria.
Ununuzi wa boti hizo, MV LINDO I na MV LINDO II, ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa TPA unaolenga kuimarisha ulinzi na usalama wa bandari, watumiaji wa huduma za bandari, meli na shehena, sambamba na kuhakikisha shughuli za biashara ya baharini na maziwa zinaendelea katika mazingira salama na yenye ufanisi.
Boti hizo zimejengwa kwa teknolojia ya kisasa na zina uwezo wa kukimbia kwa kasi ya ‘knots 35’, hali inayoziwezesha kufika kwa haraka katika maeneo yenye matukio ya dharura, kufanya doria za mara kwa mara na kuimarisha ulinzi katika maeneo ya bandari pamoja na fukwe zinazozizunguka.
MV LINDO I itatumika kufanya doria katika Bandari ya Dar es Salaam na maeneo yote ya fukwe za ukanda wake, huku MV LINDO II ikipelekwa kuimarisha ulinzi katika Bandari za Ziwa Victoria na maeneo ya fukwe zinazozihudumia.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mkurugenzi wa Huduma za Meli na Shughuli za Kibandari, Nahodha Abdulla Mwingamno, amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya TPA ya kuhakikisha bandari za Tanzania zinaendelea kuwa salama, zenye ufanisi na zinazokidhi viwango vya kimataifa.
“Kupatikana kwa boti hizi kutaimarisha usalama wa watumiaji wa bandari, meli na shehena za wateja zikiwa melini na bandarini. Aidha, zitaongeza uwezo wetu wa kufanya doria, kukabiliana na matukio ya dharura na kudhibiti vitendo vya wizi, udokozi na magendo,” amesema Nahodha Mwingamno.
Ameongeza kuwa kuimarika kwa usalama kutazidi kuongeza imani ya wafanyabiashara na wadau wa usafirishaji, kuvutia shehena nyingi zaidi kupita katika bandari za Tanzania, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuchochea ongezeko la mapato ya TPA pamoja na makusanyo ya Serikali.
Kwa mujibu wa Nahodha Mwingamno, boti hizo pia zitawawezesha askari wa TPA kupanua wigo wa doria na ulinzi katika maeneo yote ya bandari na fukwe zake, hatua itakayoongeza uwezo wa Mamlaka wa kulinda miundombinu ya kimkakati na kuhakikisha usalama wa shughuli za usafirishaji wa majini.
Ununuzi wa boti hizo ni sehemu ya maboresho yanayoendelea kufanywa na TPA katika eneo la usalama, ambapo tayari Mamlaka imeweka mfumo wa kisasa wa ufuatiliaji kupitia zaidi ya kamera 480 za ulinzi (CCTV) katika Bandari ya Dar es Salaam na nyinginezo.
TPA inaendelea kuwekeza katika teknolojia na vifaa vya kisasa ili kuhakikisha bandari za Tanzania zinabaki kuwa salama, shindani na zenye uwezo wa kuhudumia ongezeko la biashara ya ndani na ya kimataifa, sambamba na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.



