Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamehimizwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki, hekima na huruma, badala ya kufungwa na masharti ya kiufundi ya kisheria yanayoweza kukwamisha utoaji haki, hasa kwa wananchi wanyonge.

Wito huo umetolewa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 06 Julai, 2026 alipokuwa akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. 

Akizungumza katika ufunguzi huo, Mhe. Masaju amesisitiza kuwa, Ibara ya 107A(1) na (2)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza wazi kuweka mbele maslahi ya haki (interest of justice).

Amesema, kwa kuwa Mahakama ya Rufani ndiyo ngazi ya mwisho katika mfumo wa utoaji haki nchini Tanzania, hivyo inabeba dhamana kubwa ya kijamii na kiungu. “Sisi tukiwa waamuzi na uamuzi wetu ukiwa wa mwisho, ninawashauri tuendelee kutenda haki tukiwa huru kwa kuzingatia Katiba na Sheria… kwa namna ambayo masharti ya kiufundi hayatatukwamisha haki kutendeka ipasavyo,” ameeleza Jaji Mkuu.

Ameongeza kwa kusema kwamba, “Na kwa sababu sisi tunafanya maamuzi tukiwa huru, tumepewa madaraka makubwa, tunakuwa huru. Sasa mtu anayefanya maamuzi akiwa huru ana masharti mawili ya kuzingatia. Moja, azingatie Katiba na Sheria za Nchi. Lakini pia kwenye kiapo chetu kile tunahimizwa kuzingatia katiba, mila, desturi, na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tukiwa huru bila hofu, huba, chuki, wala upendeleo. Kila mtu aliye huru anapotekeleza madaraka yake, pale ambapo katiba au sheria imetamka utakuwa huru kama sisi. Kubwa la kwanza ni kuzingatia katiba na sheria za nchi.”

Aidha, Mhe. Masaju amewasisitiza Majaji hao juu ya umuhimu wa Kuzingatia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambapo amesema, Majaji na Mahakimu wametajwa bayana chini ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kama Viongozi wa umma. “Chini ya Kifungu cha 6(1)(a), Viongozi hawa wanatakiwa kuwa waaminifu (honest), wenye utu na huruma (compassion), na kufanya maamuzi kwa uhalisia na bila upendeleo (objectivity). Kadhalika, Jaji Mkuu amewataka kujituma na kuwa wepesi wa kujiongeza katika kazi (Proactive and Active).

Amesema; Majaji hawatakiwi kuwa watazamaji tu (passive) pale ambapo kumbukumbu za mashauri zinaonesha uwepo wa mapungufu yaliyo wazi. “Kwa kuwa sisi tuna kauli ya mwisho, ndio maana naomba kuwashauri Wahe. Majaji kwamba tuendelee kuwa ‘proactive’ na ‘active’, tusiwe ‘passive’. Hatua yoyote, sisi ndio tuna hilo jukumu na ndio tunawajibika. Na ikiwa kuna lawama zozote, lawama zile hazitaenda kwa Mawakili, zitaenda kwetu Mahakama. Wakati fulani wanatuita wazee, lakini kwa sasa tunafanya vizuri. Mimi ninaomba kuwahimiza tu kwamba tudumishe huo utaratibu, tabia hiyo ni njema,” amesisitiza Mhe. Masaju.

Vilevile, Jaji Mkuu amewataka Majaji hao kulinda haki ya wanyonge hususan wananchi wanaojitetea wenyewe bila Mawakili au wale ambao mashauri yao yamechukua miaka mingi tangu kuanzia Mahakama za Mwanzo.

Mbali na maslahi ya haki, Mhe. Masaju ameongeza pia kwa kuwataka Majaji hao kuzingatia maslahi ya umma pamoja na maslahi ya Taifa ambapo amesema kwenye Katiba, pamoja na kutajwa kwingineko, yametajwa pia katika Ibara ya 30(2). 

“Lakini kwa urahisi sana, kila kitu kilichokuwa kimewekwa kwenye Sheria kina maslahi ya umma, kina maslahi ya Taifa. Na ndio maana kikawekwa pale. Kwa hiyo katika mazingira kama hayo, mimi ninawaamini ninyi Waheshimiwa. Kwanza mna sifa zote za kuwa Majaji na Majaji wa Mahakama ya Rufani, mna hekima mna akili. Mtaendelea kulisaidia Taifa hili kufanya haki iendelee kutendeka katika taifa hili kwa ufanisi ipasavyo. Yazingatieni haya mafunzo,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amewasisitiza Majaji hao kujenga falsafa ya sheria za ndani (Local Jurisprudence); ambapo ameeleza kuwa, Tanzania ina miaka mingi ya uhuru na ina uwezo wa kutosha wa kisheria na ukweli wa mazingira wa kujenga misingi yake yenyewe ya kisheria, hivyo amewashauri Majaji kuacha tabia ya kukimbilia kunukuu maamuzi ya nchi za nje kama Uingereza au India na badala yake wachague kuendeleza maamuzi mazuri yaliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania ili kuweka vigezo imara vya nchi.

“Sisi tunafanya maamuzi yanayoenda kutumika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatufanyi maamuzi yatakayoenda kutumika huko India au kwingineko. Sisemi kwamba hamuwezi mkayasoma huko au hatuwezi tukayasoma yale lakini wakati fulani mimi naona tunarejea huko, lakini unaangalia mbona hata hii Mahakama ya kwetu hapa ilishaamua kitu kama hiki?” ameeleza Jaji Mkuu.

Ameongeza kwa kuwakumbusha juu ya Matumizi ya Hekima na Akili; ambapo amesema kuwa, ingawa utaalamu wa sheria ni muhimu, matumizi ya akili ya kuzaliwa na hekima ni vitu vya thamani zaidi vinavyomsaidia Jaji kutoa uamuzi wa haki bila hofu, huba, chuki, wala upendeleo.

Vilevile, Jaji Mkuu amewakumbusha Majaji hao kuwa wao ni watumishi wa Mungu, hivyo wawe na amani ambapo amesisitiza kwa kusema, “hamuwezi mkasema ninyi si watumishi wa Mungu wakati mnafanya kazi ya Mungu. Ninyi ni sehemu ya Serikali, ni watumishi wa Mungu na hata hivyo mnafanya kazi zake. Hata kama ninyi sio Mungu. Kwa hiyo hamuwezi mkasema kwamba ninyi si watumishi wa Mungu. Sasa kama si watumishi wa Mungu mnataka kuwa watumishi wa mashetani? Na tukishakuwa watumishi wa mashetani hizo kazi tutazitenda? Ninavyozungumza kuwa watumishi wa Mungu ni katika muktadha wa kwamba mnafanya kazi za Mwenyezi Mungu. Na tunaofanya kazi ya Mwenyezi Mungu, moja lazima tuwe wanyenyekevu sana.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake endelevu za kuimarisha Mhimili huo kupitia uboreshaji wa miundombinu, vitendea kazi, na kuongeza rasilimaliwatu (Majaji na watumishi wa Kada nyingine huku akibainisha kuwa Rais Samia anaiishi kwa vitendo kauli yake ya kutaka kuifikisha Mahakama ya Tanzania katika hadhi ya Kimataifa.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amekishukuru Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto chini ya Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo-Jaji wa Mahakama ya Rufani, amemshukuru Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani na Viongozi wote wa kada ya Utawala na sheria kwa ushirikiano wao katika kufanikisha mafunzo hayo yanayoendeshwa kwa njia shirikishi na kirafiki.

Mafunzo hayo yaliyosheheni mada mbalimbali yamewakusanya pamoja Majaji hao wapya wa Mahakama ya Rufani kwa lengo la kuwaandaa kuanza kutekeleza majukumu yao katika ngazi hiyo ya juu ya utoaji haki.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 06 Julai, 2026 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 06 Julai, 2026 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kushoto kwa Jaji  Mkuu ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo Elekezi iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) leo tarehe 06 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Sehemu ya Viongozi na Watumishi wengine wa Mahakama na IJA walioshiriki katika ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo hayo leo tarehe 06 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Majaji wapya tisa wa Mahakama ya Rufani (waliosimama). Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania (waliosimama) walioshiriki kwenye ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 06 Julai, 2026. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto (waliosimama) walioshiriki kwenye ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani leo tarehe 06 Julai, 2026. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)