Na Timothy Mwakyenda – MAELEZO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa mafanikio ya Tamasha la Lugha ya Kiswahili lililofanyika nchini Ufaransa yamefungua ukurasa mpya wa kuitangaza lugha ya Kiswahili duniani na kuifanya kuwa nyenzo muhimu ya kukuza uchumi, biashara na diplomasia ya Tanzania.
Akizungumza Julai 8, 2026, alipotembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Msigwa amesema kuwa ushiriki wa Tanzania katika tamasha hilo umeonyesha kuwa Kiswahili sasa si lugha ya mawasiliano pekee, bali ni rasilimali yenye uwezo wa kufungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania.
Msigwa ameendelea kusema kuwa mataifa mengi yaliyofanikiwa kiuchumi yamenufaika pia kwa kutumia lugha zao kama chachu ya biashara na ubunifu, hivyo Watanzania wanapaswa kukitumia Kiswahili kama nyenzo ya kutangaza bidhaa, huduma na utamaduni wao katika soko la kimataifa.
” Baada ya mafanikio ya tamasha hilo, taasisi za Serikali na sekta binafsi zinapaswa kujipanga kimkakati ili kutumia fursa zinazotokana na kuongezeka kwa matumizi ya Kiswahili duniani, hatua itakayochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yenye lengo la kujenga uchumi wa dola za Marekani trilioni moja”, amesisitiza Msigwa.
Akihusisha ujumbe huo na Maonesho ya Sabasaba, Msigwa amefafanua kuwa maonesho hayo yanatoa jukwaa muhimu la kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa za ndani, ubunifu wa teknolojia na uongezaji thamani wa mazao, akitaja mfano wa vijana wa DIT ambao wametengeneza bajaji ya umeme na wafanyabiashara wanaochakata mazao kama korosho na parachichi na kusisitiza kuwa maendeleo hayo yanapaswa kuungwa mkono ili kuongeza ajira, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuhakikisha fedha nyingi zaidi zinabaki kuzunguka ndani ya uchumi wa Tanzania.
Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi kwa kuelekeza nguvu katika uzalishaji, biashara, kilimo, viwanda na ubunifu badala ya kushawishiwa na ajenda zinazoweza kuvuruga maendeleo ya Taifa.
Sambamba na hilo amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea Maonesho ya Sabasaba ili kujifunza teknolojia mpya, kupata maarifa kutoka kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi na kutumia fursa hizo kuboresha shughuli zao za kiuchumi huku akibainisha kuwa ongezeko la idadi ya nchi na kampuni zinazoshiriki katika maonesho ya mwaka huu ni ishara ya kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Ambapo, maarifa, teknolojia na lugha ya Kiswahili vinatajwa kuwa ni miongoni mwa nyenzo muhimu zitakazoifanya Tanzania kufikia malengo yake ya maendeleo.








