Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Dar es Salaam

Zao la mkonge linaendelea kuwa moja ya mazao yenye fursa kubwa za kiuchumi nchini Tanzania. Kwa mujibu wa Bodi ya Mkonge Tanzania, uzalishaji wa sasa ni takribani tani 72,000 kwa mwaka, wakati mahitaji ya soko la dunia yanafikia tani 500,000 hadi 600,000 kwa mwaka, jambo linaloonyesha nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji na uwekezaji.

Akizungumza Julai 8,2026 katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Masoko wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Best Rukanda, amesema Tanzania ina mazingira mazuri ya kilimo cha mkonge, hasa katika mikoa ya Tanga na Morogoro.

Ameeleza kuwa mkonge hutumika kutengeneza kamba, mikoba, viatu, mazulia, karatasi maalumu na hata noti, hivyo kuwa zao muhimu kwa maendeleo ya viwanda na uchumi wa Taifa.

Aidha, amesema soko kubwa la mkonge wa Tanzania lipo China, huku barani Afrika masoko makuu yakiwa Nigeria, Ghana, Morocco, Misri na nchi nyingine za Afrika Magharibi.

Bodi ya Mkonge imewahimiza Watanzania na wawekezaji kutumia fursa zilizopo katika uzalishaji na uchakataji wa zao hilo ili kuongeza tija, ajira na mapato ya taifa kupitia fedha za kigeni.