Msalala, Kahama
Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi imepitia na kujadili Mpango wa Ufungaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, ili kujiridhisha kama unakidhi matakwa ya sheria, kanuni na miongozo inayosimamia shughuli za ufungaji migodi nchini.
Kikao hicho kilichofanyika mapema jana kililenga kutathmini iwapo mpango huo unazingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, Kanuni za Uchimbaji Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za mwaka 2010 pamoja na Mwongozo wa Ufungaji Migodi wa mwaka 2019.
Akiongoza kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi, Mhandisi Hamisi Kamando, alisema migodi ya kati na mikubwa inalazimika kisheria kuandaa na kuwasilisha mipango ya ufungaji migodi kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi kwa ajili ya mapitio na uidhinishaji.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123 na Kanuni ya 206 ya Kanuni za Uchimbaji Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za mwaka 2010, kila mmiliki wa mgodi anatakiwa kuandaa mpango wa ufungaji wa mgodi na kuuwasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi ili ufanyiwe mapitio ya kitaalam kabla ya kuidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi.
Mhandisi Kamando alieleza kuwa jukumu la Kamati hiyo ni kupitia na kuidhinisha mipango ya ufungaji migodi ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinapofikia mwisho, maeneo ya migodi yanarejeshwa katika hali salama na inayokubalika kimazingira, huku maslahi ya jamii zinazozunguka migodi yakilindwa.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Madini, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tume ya Madini pamoja na viongozi wa Mkoa wa Shinyanga na Wilaya ya Kahama.
Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, Agapith Paul, aliishukuru Kamati kwa maoni na ushauri uliotolewa, akisema utasaidia kuboresha Mpango wa Ufungaji wa Mgodi huo.
Alisisitiza kuwa mgodi utaendelea kushirikiana kwa karibu na Kamati pamoja na kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa kwa maslahi ya mgodi, jamii na Taifa kwa ujumla.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Kamishna wa Polisi Salum Rashid Hamduni, alisema migodi imeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya mkoa huo kwa kuchangia ajira kwa vijana, kuongeza fursa za biashara kwa wazabuni na wakandarasi wazawa, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aliahidi kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itaendelea kushirikiana na Mgodi wa Bulyanhulu katika kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendelea kwa kuzingatia maslahi ya wananchi, mazingira na Serikali.




