Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, amezitaka kampuni za wazawa zinazotekeleza miradi ya kusambaza umeme vitongojini kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kujijengea uwezo wa kushindana kimataifa na kupata miradi nje ya nchi.
Akizungumza mkoani Singida Julai 16, 2026 katika kikao na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kusambaza umeme vitongojini mkoani humo, Balozi Kingu alisema miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekelezwa na kampuni za ndani pamoja na baadhi ya kampuni za kigeni, hivyo ni muhimu kwa kampuni za wazawa kutumia fursa hiyo kujenga rekodi nzuri ya utendaji.
Alisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wa vitongojini wanapata huduma ya umeme kwa wakati, hivyo wakandarasi wote wanapaswa kukamilisha miradi ndani ya muda uliopangwa.
Aidha, alionya kuwa Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Balozi Kingu pia aliwataka wasimamizi wa miradi ya REA kushirikiana kwa karibu na mamlaka mbalimbali katika maeneo ya utekelezaji wa miradi ili kurahisisha kazi na kulinda miundombinu.
Vilevile, aliwataka kuhakikisha wanawasilisha taarifa za maendeleo ya miradi kwa Kamati za Ulinzi na Usalama katika kila hatua ya utekelezaji ili changamoto zozote zitakazojitokeza ziweze kushughulikiwa kwa wakati.
Kwa upande wao, wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo mkoani Singida waliahidi kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na kuhakikisha miradi inakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Mhandisi wa Miradi wa China Railway Group Engineering Ltd, Baraka Mhagama, alisema kampuni hiyo inaendelea na utekelezaji wa mradi wa HEP IIB katika wilaya zote tano za Mkoa wa Singida na imejipanga kukamilisha kazi kwa viwango vinavyohitajika.
Naye Mhandisi wa Miradi wa kampuni ya wazawa ya Transpower Ltd, Shaibu Kizee, alisema wamepokea maelekezo ya Serikali na wataendelea kufanya kazi kwa weledi na ufanisi, wakiamini kuwa utendaji mzuri utawapa fursa ya kushindana na kupata miradi katika nchi nyingine.



