Wananchi na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendesha zoezi la usafi lililofanyika sokoni hapo, wakisema limechangia kuboresha mazingira ya biashara, afya ya jamii na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.

Zoezi hilo lilifanyika Julai 29, 2026, chini ya uongozi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Kaster Ngonyani. Akizungumza wakati wa zoezi hilo, amesema shughuli hiyo ni sehemu ya kampeni endelevu ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika utunzaji wa mazingira na kuhakikisha maeneo ya biashara yanakuwa safi na salama.

SACP Ngonyani amewataka wafanyabiashara na wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudumisha usafi wa soko pamoja na maeneo mengine yanayowazunguka, akisisitiza kuwa mazingira safi huchangia afya bora na maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kashaulili, Johari Korongo, amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kwa kuonyesha ushirikiano mzuri na wananchi kupitia shughuli za kujitolea kwa manufaa ya jamii. Amesema hatua hiyo ni mfano wa kuigwa na kuzitaka taasisi nyingine kujitokeza kushiriki shughuli za maendeleo na utoaji wa huduma kwa jamii.