Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Matumizi ya teknolojia ya kidijitali yanaendelea kubadilisha sekta ya kilimo nchini, huku Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ikieleza kuwa imebuni na kuendeleza mifumo mbalimbali inayorahisisha huduma za Serikali, kuimarisha uwazi na kuongeza tija kwa wakulima na taasisi za umma.
Akizungumza leo Agost 2,2026 katika Maonesho ya 88 ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Subira Kaswaga, amesema mamlaka hiyo imejikita kuhakikisha taasisi za Serikali zinatumia mifumo ya kidijitali ili wananchi wapate huduma kwa haraka, kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.
Amesema kupitia ushirikiano na Wizara ya Kilimo, e-GA imeunda mfumo wa e-Kilimo, unaowezesha ukusanyaji wa taarifa za wakulima, usimamizi wa taasisi zilizo chini ya wizara pamoja na utoaji wa vibali mbalimbali vinavyohusu shughuli za kilimo.
Kaswaga amesema e-GA pia imeungana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kutengeneza mfumo wa kidijitali unaorahisisha usimamizi wa vyama vya ushirika, ambapo wakulima wanaweza kufuatilia masoko ya mazao yao, mwenendo wa mauzo na kupata taarifa zinazoongeza uwazi katika shughuli za ushirika.
Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), mamlaka hiyo imeanzisha Mfumo wa Usimamizi wa Mbolea (Fertilizer Information System – FIS) unaowezesha usajili wa wazalishaji na waagizaji wa mbolea, pamoja na kufuatilia bei elekezi ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa urahisi na kwa gharama stahiki.
Aidha, amesema e-GA imeendelea kuunganisha taasisi mbalimbali za Serikali kupitia mifumo ya kidijitali, hatua inayorahisisha ubadilishanaji wa taarifa na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kufika katika banda la e-GA ili kujifunza kuhusu mifumo mbalimbali ya kidijitali inayotumiwa serikalini na namna inavyochangia kuboresha huduma na maendeleo ya sekta mbalimbali nchini.



