Na Saidina Msangi, WF, Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Africa50 Bw. Alain Ebobisse, amebainisha kuwa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM) pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), ni fursa ya kuonesha mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika sekta ya miundombinu, kutangaza fursa zinazopatikana ikiwa ni ushahidi kuwa uwekezaji katika miundombinu ya Afrika una tija, unalipa na unaweza kufadhiliwa.

Bw. Ebobisse alisema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi, Khamis Mussa Omar (MB), katika kikao cha pamoja cha maandalizi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Bw. Ebobisse alibainisha kuwa ajenda kuu ya mkutano huo itakuwa ni ujenzi wa uchumi wa viwanda barani Afrika kupitia uongezaji thamani wa rasilimali za ndani, jambo linalotegemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa nishati ya uhakika huku akipongeza dira ya uongozi wa Tanzania katika kuvutia mtaji wa sekta binafsi.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana maono makubwa ya kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta ya miundombinu nchini Tanzania. Sisi Africa50 ni mojawapo ya nyenzo zinazosaidia kutekeleza maono hayo kwa kushirikiana katika utekelezaji wa miradi, ambapo miundombinu mbalimbali ikiwemo nishati ni muhimu katika maendeleo ya viwanda na kutuma ujumbe kuwa Afrika iko tayari kwa uwekezaji,” alisema Bw. Ebobisse.

Bw. Ebobisse aliongeza kuwa Africa50 imeweka kipaumbele kikubwa katika miundombinu ya gesi asilia ikiwemo mabomba na mitambo ya uchakataji ili kuelekeza gesi zaidi kwenye maeneo ya viwanda nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla ili kuongeza thamani ya rasilimali na kuimarisha uchumi wa Afrika.

Alisisitiza kuwa licha ya uwepo wa kundi kubwa la wawekezaji tayari wenye hamasa ya kushiriki, huo ulikuwa wakati muafaka wa kutuma ujumbe kwa Tanzania, Afrika na dunia nzima kwamba Bara la Afrika liko tayari na ni eneo salama na la kimkakati kwa uwekezaji wa miundombinu.

Naye Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi, Khamis Mussa Omar (MB), alisema kuwa Serikali imekamilisha maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Miundombinu Afrika unaolenga kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika miundombinu ya kimkakati, ikiwemo gesi asilia, umeme na viwanda barani Afrika.

Alisema Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM) pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), utakaofanyika tarehe 5 na 6 Agosti, 2026 katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), Dar es Salaam unatarajiwa kufunguliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tunatarajia kusaini hati tatu za mashirikiano katika afya hasa usafishaji wa damu (dialysis), tumefanya tathmini ya maendeleo ya miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa gesi asilia, miundombinu ya usafirishaji wa nishati, pamoja na masuala mengine ya nishati yanayolenga kuharakisha maendeleo ya uchumi wa viwanda, ” alisema Mhe. Balozi Omar.

Balozi Omar alithibitisha kuwa Serikali imejiridhisha kuwa maandalizi yote muhimu ya mkutano huo unaotarajiwa kukutanisha viongozi wa kitaifa, marais wa taasisi za kifedha, na wawekezaji wakubwa wa kimataifa yako tayari ili kuhakikisha mkutano huo wa siku mbili unapata mafanikio makubwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.