Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wameongezeka kwa 4,881 ndani ya miaka minne, kutoka 13,074 mwaka wa masomo 2021/22 hadi kufikia 17,955 mwaka 2025/26, huku chuo hicho kikieleza kuwa ongezeko hilo limechochewa na uwekezaji mkubwa katika miundombinu na upanuzi wa programu za masomo.

Aidha katika kukidhi mahitaji ya ongezeko hilo, Chuo hicho kimetekeleza jumla ya miradi 27 ya maendeleo yenye thamani ya takribani Sh bilioni 15.66 katika mwaka wa fedha 2025/26, ikilenga kuboresha mazingira ya kufundishia, kujifunzia, utafiti na utoaji wa huduma kwa jamii.

Hayo yameelezwa leo Agosti 04,2026 jijini Dodoma na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Prof.William Mwegoha wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na maelekeo wa taasisi hiyo.

Ameeleza Chuo hicho ambacho ni taasisi ya umma chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kimeendelea kupanua wigo wa utoaji elimu ambapo kwa sasa kinatoa programu takribani 100 kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada, shahada ya awali, shahada ya umahiri hadi shahada ya uzamivu.

“Miradi iliyotekelezwa imehusisha Kampasi Kuu Morogoro, Kampasi ya Mbeya na Kampasi ya Dar es Salaam, ikiwemo ujenzi na ukamilishaji wa majengo ya taaluma na utawala, madarasa janja, studio ya kisasa ya kutengeneza maudhui ya kufundishia kwa njia ya mtandao, ukarabati wa hosteli za wanafunzi, vituo vya afya na miundombinu ya maji,”amesema

Licha ya hayo ameeleza kupitia mradi wa HEET, Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea na ujenzi wa madarasa na kumbi za mihadhara, kituo cha TEHAMA pamoja na miundombinu ya maji na majitaka katika Kampasi Kuu Morogoro. Pia, mradi huo umehusisha ujenzi wa majengo ya madarasa, hosteli za wanafunzi, nyumba za watumishi, kituo cha afya na bwalo la chakula katika kampasi mpya ya Tanga.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, chuo kimepanga kutekeleza miradi yenye thamani ya Sh bilioni 4.83 kupitia fedha za ndani, ikiwemo kuendelea na ujenzi wa jengo la taaluma Kampasi ya Dar es Salaam Tegeta, maboresho ya vituo vya afya, ukarabati wa nyumba za watumishi, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA na kuimarisha tafiti za kitaaluma ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI).

Prof.Mwegoha amesema eneo la TEHAMA, chuo kimeongeza uwezo wa mtandao kutoka Mbps 650 hadi Mbps 1,140 katika kampasi zake zote tatu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuwezesha programu nyingi zaidi kufundishwa kwa njia ya mtandao.