Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Sudani Kusini, Mhe. Clement Juma Mbugoniwia, ametembelea banda la Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea Nzuguni, mkoani Dodoma, kwa lengo la kujifunza mifumo inayotumika nchini katika kudhibiti na kuthibitisha ubora wa mbegu.
Waziri huyo akiwa ameambatana na mwenyeji wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, alielezwa namna TOSCI inavyotekeleza jukumu lake la kuhakikisha mbegu zinazozalishwa na kusambazwa kwa wakulima zinakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Bw. Nyasebwa Chimagu, amesema taasisi hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali ya Sudani Kusini katika kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ubora wa mbegu, pamoja na kukuza uzalishaji na biashara ya mbegu bora za mazao ya kilimo.

Chimagu amesema miongoni mwa mifumo inayotumika na TOSCI ni mfumo wa kielektroniki wa uhakiki wa ubora wa mbegu kupitia lebo maalum za ubora. Mfumo huo unamwezesha mkulima kuhakiki uhalali na ubora wa mbegu alizonunua kwa kutumia simu ya kiganjani, kwa kuingiza namba maalum inayopatikana baada ya kukwangua lebo na kufuata maelekezo kupitia 14852#.
Amesema mkulima anaweza pia kupata huduma kwa kuwasiliana na TOSCI kupitia namba ya huduma kwa wateja isiyolipiwa 0800782424, hatua inayolenga kuongeza uelewa na uwezo wa wakulima katika kutambua mbegu zilizothibitishwa.
Katika ziara hiyo, viongozi hao pia walipata ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa mbegu za awali, maarufu kama Early Generation Seed, ambazo ni muhimu katika mnyororo wa uzalishaji wa mbegu bora.
Kwa mujibu wa Chimagu, TOSCI inashirikiana na taasisi za utafiti, ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), pamoja na sekta binafsi, katika kutambua na kuthibitisha aina mpya za mbegu kwa kuzingatia mahitaji ya soko na mazingira ya wakulima.

Aidha, amesema TOSCI inazingatia viwango vya kimataifa vya ISTA na OECD katika utekelezaji wa majukumu yake ya udhibiti na uthibitishaji wa ubora wa mbegu.
Amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Sudani Kusini katika eneo hilo unaweza kusaidia kubadilishana uzoefu na maarifa kuhusu mifumo ya udhibiti wa ubora wa mbegu, pamoja na kuimarisha uzalishaji na biashara ya mbegu bora katika masoko ya ndani na kimataifa.




