Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

WAKULIMA nchini wamehimizwa kujiunga na Bima ya Kilimo ili kujikinga dhidi ya hasara zinazotokana na majanga ya asili, magonjwa na wadudu waharibifu, hatua itakayowasaidia kulinda uwekezaji wao na kuendelea na uzalishaji hata wanapokumbwa na changamoto.

Wito huo umetolewa katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma na Afisa Bima wa NIC Insurance, Aman Mollel, ambapo amesema bima hiyo imebuniwa kuwakinga wakulima dhidi ya athari za ukame, mafuriko, magonjwa ya mimea, wadudu waharibifu, vimbunga na mvua ya mawe.

Amesema mazao yanayoweza kukatiwa bima ni pamoja na pamba, korosho, kahawa, tumbaku, maharage, mahindi, mpunga, shayiri, alizeti na chai.

Mollel amefafanua kuwa ili mkulima aweze kupata huduma hiyo anatakiwa kujaza na kusaini fomu ya maombi, kuwasilisha taarifa za gharama za uzalishaji kwa hekta, makadirio ya gharama au bei ya mazao pamoja na taarifa za kihistoria za uzalishaji.

“Bima ya Kilimo ni kinga ya mkulima dhidi ya majanga, hasara na changamoto zinazoweza kujitokeza katika uzalishaji wa mazao,” amesema.

Aidha, amesema NIC Insurance pia inatoa Bima ya Mifugo inayowalinda wafugaji dhidi ya hasara zinazotokana na vifo vya mifugo vinavyosababishwa na magonjwa, ajali, wizi au uchinjaji wa lazima unaofanywa kwa ushauri wa daktari wa mifugo.

Amesema bima hiyo inapatikana kwa ng’ombe wa maziwa, ng’ombe wa nyama, kuku na mbuzi, ambapo mwombaji anatakiwa kuwasilisha fomu ya maombi iliyosainiwa, ripoti ya ukaguzi kutoka kwa afisa mifugo na ratiba ya chanjo.

“Matumizi ya bima yanasaidia kukuza uwekezaji katika sekta ya kilimo na mifugo, kuwawezesha wakulima na wafugaji kurejea katika uzalishaji baada ya kupata hasara, pamoja na kuongeza fursa ya kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha kwa masharti nafuu,” amesema.

Amewahimiza wakulima na wafugaji wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kufika katika banda la NIC Insurance ili kupata elimu kuhusu huduma za bima na namna zinavyoweza kulinda uwekezaji wao dhidi ya majanga mbalimbali.