Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

CHUO cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT Academy) kimefungua dirisha la udahili kwa programu zake za muda mrefu na mfupi, huku kikiwahamasisha vijana waliomaliza kidato cha sita, wahitimu wa vyeti na shahada pamoja na watumishi wa sekta ya fedha kuchangamkia fursa hiyo ili kujenga wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sekta ya fedha.

Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, Assintant Manager – Professional Certifications and Short Courses wa Chuo cha Benki Kuu, Tulla Mwigune, amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1961 kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Benki Kuu, lakini kwa sasa kimepanua wigo wake na kuhudumia wafanyakazi wa benki, taasisi za fedha na wanafunzi kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Amefafanua kuwa, miongoni mwa programu zinazotolewa ni Ordinary Diploma in Banking Practice and Supervision, inayofundishwa kwa miaka miwili katika kampasi ya Mwanza kwa wahitimu wa kidato cha sita na wenye vyeti vya fani mbalimbali za biashara.

“Waombaji wa kidato cha sita wanatakiwa kuwa na angalau Principal Pass moja na Subsidiary Pass moja, huku wenye elimu ya kidato cha nne wakitakiwa kuwa na cheti katika fani kama uhasibu, benki, fedha, masoko, ununuzi na ugavi, usimamizi wa rasilimali watu, teknolojia ya habari au utawala wa biashara,” amesema.

Amebainisha kuwa, ada za programu hiyo zimewekwa katika kiwango nafuu, ambapo mwanafunzi hulipa Sh milioni 1.35 kwa mwaka wa kwanza na Sh milioni 1.25 kwa mwaka wa pili, huku malipo yakiruhusiwa kufanywa kwa awamu zisizozidi tatu.

Aidha, amesema chuo kinatoa Postgraduate Diploma in Banking Management katika kampasi ya Dar es Salaam kwa wahitimu wa shahada ya kwanza kutoka fani yoyote, ambapo masomo hufanyika nyakati za jioni ili kuwawezesha watumishi kuendelea na majukumu yao ya kazi sambamba na masomo.

“Dirisha la udahili kwa sasa liko wazi na waombaji wanaweza kuwasilisha maombi kupitia tovuti yetu ya chuo,” amesema.

Ameeleza kuwa moja ya nguvu ya chuo hicho ni kutumia mfumo wa ufundishaji unaozingatia umahiri (competence-based learning), unaochanganya nadharia na uzoefu wa vitendo unaotolewa na wataalamu wa Benki Kuu na sekta ya fedha.

Mbali na programu za muda mrefu, amesema Chuo cha Benki Kuu kinaendelea kutoa kozi mbalimbali za muda mfupi zinazochukua kati ya wiki moja na tatu katika maeneo ya benki, fedha na huduma za kifedha kwa watumishi wanaotaka kuongeza ujuzi wao.

“Nitoe wito kwa wahadhiri na wakufunzi wa masuala ya fedha kujiunga na programu ya Certified Financial Trainer, inayotolewa kwa muda wa wiki mbili kila robo mwaka kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwapa ithibati ya kitaaluma katika kufundisha masuala ya fedha,” amesema.

Amesisitiza kuwa mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Benki Kuu yanalenga kuzalisha wataalamu wenye uelewa wa kinadharia na uzoefu wa vitendo unaohitajika katika sekta ya fedha, benki na uchumi.